SERIKALI YAAHIDI TAA ZA BARABARANI KUPUNGUZA AJALI KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 1 September 2025

SERIKALI YAAHIDI TAA ZA BARABARANI KUPUNGUZA AJALI KAHAMA



Na Neema Nkumbi - Huheso Digital Kahama


Serikali wilayani Kahama kupitia Jeshi la Polisi imejipanga kusimika taa za kuongozea magari katika maeneo ya Lumambo, Bijampora na Phantom, ili kupunguza msongamano na ajali zinazochangiwa na ukosefu wa mwongozo rasmi wa vyombo vya moto.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika majengo manispaa ya Kahama, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa serikali kutatua changamoto za miundombinu ya barabara katika kata 18 za Manispaa ya Kahama, huku akiongeza kuwa serikali pia imejipanga kuweka tuta katika eneo la Shunu, ambalo limekuwa likigharimu maisha ya wananchi kutokana na ukosefu wa alama za barabarani.


Hata hivyo, baadhi ya wananchi wameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa barabara hizo ambapo Hidaya Melkiory, mkazi wa Kahama, alihoji juu ya kusuasua kwa mradi huo, akieleza hofu kuwa mvua zinakaribia kuanza mwezi Septemba barabara na mitaro iliyopo inaweza kuharibika zaidi.


“Mvua zikianza je barabara zitakuwa zimekamilika? Wanaenda polepole sana, hii italeta kero zaidi ya mwanzo,” amesema.


Dc Nkinda amesema Serikali imejizatiti kukamilisha ujenzi wa barabara za mjini Kahama kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometer 12 kifikia Novemba 2025 licha ya kuwepo kwa changamoto za kiutekelezaji katika mradi huo mkandarasi ameahidi kukamilisha mradi



“Mheshimiwa Rais ametuletea fedha mwaka wa fedha uliopita na tukafuata taratibu za kumpata mkandarasi, Ni kweli kulikuwa na malalamiko kuwa ujenzi unasuasua, lakini tumekutana na mkandarasi na ametuhakikishia kufikia Novemba barabara zitakuwa zimekamilika,” amesema Nkinda.


Kwa upande wake, Aman Omary ameeleza kero za barabara zinazopitika kwa shida wakati wa mvua katika maeneo ya shule za Nyashimbi, Mama Samia na Majengo, akisema mitaro inayoendelea kujengwa tayari imeanza kukatika kabla ya mradi kukamilika.


Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Kahama, Mhandisi Joseph Mkwizu, amesema marekebisho yanaendelea kulingana na bajeti za kila mwaka na kueleza kuwa maandalizi ya kazi ya lami yameshaanza.



“Ni matarajio yetu kuwa mitaro yote itajengwa kwa viwango vinavyohitajika na tutaingia kwenye hatua ya lami, Mitambo ya lami tayari imefungwa na kokoto zimeanza kuzalishwa,” amesema Mkwizu.






No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso