
Na Neema Nkumbi- Huheso Digital Kahama
Mgogoro wa muda mrefu kuhusu mipaka ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mwanva kilichopo Manispaa ya Kahama, sasa umepatiwa ufumbuzi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, amewataka wananchi waliokuwa wamesahaulika katika takwimu alizopewa hayati Dkt. John Magufuli kuwa eneo la ekari 40 ndilo litakalobaki katika mipaka ya chuo hicho, waendelee na shughuli zao za ujenzi na maendeleo kwenye maeneo yao, huku akisisitiza kuwa wale waliovamia eneo hilo baada ya kauli ya hayati Magufuli, sheria itachukua mkondo wake.
Akizungumza kwa njia ya simu kupitia Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, Waziri Ndejembi amesema atatuma timu ya wataalamu kuja kuhakiki ili kila mwenye haki apate haki yake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Mhita amewataka wananchi kuwa na amani kwani changamoto hiyo sasa imepata mwarobaini, na akawahakikishia kuwa wako huru kuendeleza maeneo yao.
Wananchi waliozungumza mara baada ya maelekezo ya waziri wametoa shukurani na pongezi zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mmoja wa wananchi, Paul Andrea, amesema: "Tunamshukuru sana Rais Samia, zamani tulikuwa tunaitwa matapeli, sasa tuko huru."
Aidha, mstaafu wa Jeshi la Magereza, Mzee Gregory Kachemba, ameonyesha furaha yake kwa hatua hiyo, akisema alimaliza mafao yake ya kustaafu kwa kujenga nyumba na kuanzisha maendeleo katika eneo hilo, hivyo kupata suluhisho la mgogoro huo ni faraja kubwa kwake.
No comments:
Post a Comment