MTHIBITI UBORA WA SHULE AWATAKA WAZAZI KUFUATILIA MAENDELEO YA WATOTO SHULENI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 1 September 2025

MTHIBITI UBORA WA SHULE AWATAKA WAZAZI KUFUATILIA MAENDELEO YA WATOTO SHULENI




Na Neema Nkumbi - Huheso Digital Kahama

Mthibiti Ubora wa Shule wilayani Kahama Athuman Abeid amewataka wazazi kutotupilia mbali jukumu lao la kufuatilia maendeleo ya kielimu na malezi ya watoto, akisisitiza kuwa dunia ya sasa inakabiliwa na changamoto kubwa za maadili.

Akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba katika shule ya Greenstar, Mthibiti huyo alisema kuwa wazazi wengi wamekuwa na shughuli nyingi kiasi cha kutojua mustakabali wa watoto wao shuleni.


“Dunia imechafuka sana kimaadili. Ukimkabidhi mtoto shule kuanzia awali hadi anahitimu darasa la saba, ni miaka zaidi ya nane. Kama hukufuatilia maendeleo yake, na iwapo walimu waliteleza, kazi ya kurekebisha itabaki kwako mzazi. Hivyo nawasihi tusijisahau, tushirikiane na walimu kwa manufaa ya baadaye ya watoto wetu,” alisema.

Kwa upande mwingine, aliwataka wahitimu wa darasa la saba kutambua kuwa safari ya elimu ndio kwanza inaanza. Alisisitiza kuwa licha ya sherehe za mahafali, wajibu mkubwa wa mtihani unaowakabili unapaswa kupewa kipaumbele.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa shule za Greenstar Daniel alitangaza kuwa taasisi hiyo kwa sasa inamiliki shule mbili za sekondari – ya wavulana na ya wasichana. Alitoa ombi kwa ofisi husika kubadilisha jina la shule ya sekondari ya Sister Irene na kuifanya Greenstar Boys, akieleza kuwa mchakato huo unapaswa kukamilika kabla ya Januari.


“Naomba wazazi muwe mstari wa mbele kuhakikisha watoto wenu wanarudi kuendelea na masomo yao hapa. Tunataka jina jipya lifahamike mapema,” alisema Mkurugenzi.

Aidha, mmoja wa wazazi waliohudhuria alitoa shukrani kwa walimu kwa kusimamia vyema taaluma na malezi ya watoto wao.


“Tunawashukuru walimu kwa juhudi kubwa za kuwalea na kuwafundisha watoto wetu. Tumewaona watoto wetu wakibadilika na kukua kielimu na kimaadili,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso