SULTAN MITIMINGI AUNGANA NA WANAWAKE WA SUPER WOMEN KAKOLA: ACHANGIA ZAIDI YA MILIONI 4 KATIKA SHEREHE YA KIKUNDI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 1 July 2025

SULTAN MITIMINGI AUNGANA NA WANAWAKE WA SUPER WOMEN KAKOLA: ACHANGIA ZAIDI YA MILIONI 4 KATIKA SHEREHE YA KIKUNDI


Mganga wa tiba asili Sultan Mitimingi akizungumza katika usiku wa kikundi cha Super Women kilichopo kata ya Bulyanhulu kijiji cha Kakola mara baada ya kukabidhi kitita cha fedha kwa ajili ya kuunga mkono maendeleo ya kikundi hicho.

NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAKOLA KAHAMA

Katika kusherehekea mafanikio na mshikamano wa wanawake, kikundi cha Super Women kilichopo Kakola kimefanya hafla maalum iliyohudhuriwa na wadau mbalimbali, akiwemo mtabibu mashuhuri wa tiba asilia, Sultan Mitimingi, ambaye alijitokeza kwa kishindo na kutoa mchango mkubwa wa vifaa na fedha.


Katika tukio hilo lililojaa hamasa na upendo, Sultan Mitimingi amechangia kikundi hicho shilingi milioni 1 taslim, ahadi ya viti 120 vya plastiki, pamoja na tenti moja lenye thamani ya shilingi milioni 1.5 – mchango unaofikia zaidi ya shilingi milioni 4 kwa jumla.


Mitimingi ambaye ni mtaalamu wa tiba asili yupo wilayani Kahama kwa ajili ya shughuli za kiganga, ameungana na akina mama hao baada ya kupata mwaliko mchana wa Juni 30, 2025, kutokana na heshima baina yake na akina mama hao.


"Akina mama wenye hiki kikundi nawaheshimu na ndio maana niko hapa, mimi naisha Dar ila huku nilikuja kwa kazi zangu za du'a na tiba na najisikia vizuri kwani najiona napendwa na niko kwenye mioyo ya watu" Amesema Mitimingi


"Nawaasa vijana wenzangu tujitume na tufanye kazi, mimi nafanya kazi muda mwingi sana nalala kidogo, na kijana atakayenifata kuniomba ushauri simnyimi, ila vijana waache uvivu wajichanganye" Ameongeza


Amewaasa vijana kuepuka mikopo umiza inayotolewa mtaani badala yake watumie fursa za mikopo inayotolewa na serikali ili wajikwamue kiuchumi huku akieleza kuwa naye yuko mbioni kuanzisha mikopo itakayozingatia masharti ya uislamu kwa ajili ya kuinua vijana.


Mgeni rasmi katika sherehe hiyo Matani Kishepo amechangia viti 100, huku wapambe wake wakichangia viti 80 na shilingi laki sita ambapo jumla ya viti vilivyochangiwa ni 300 pamoja na alivyochangia Mitimingi.


Julieth Appolinary ni mwenyekiti wa kikundi cha Super Women, amesema kuwa sherehe hiyo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kupongezana na kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kusaidia kukuza shughuli za kikundi.



Ametoa shukrani za dhati kwa wageni wote walioshiriki, huku akimpongeza Matani Kishepo kwa hatua ya kumualika Sultan Mitimingi, ambaye amekuwa mchango mkubwa kwa kikundi chao mwaka huu.


"Huu ni mwaka wa tatu tunafanya sherehe hii, na mwaka huu tuliona ni vyema kumwalika mtu mkubwa hapa Tanzania Sultani Mitimingi, maana tunamfatilia kwenye mitandao ya kijamii na kazi zake tunaziona" Amesema Julieth


"Kwa kweli Mitimingi tulikutana nae Hotelini kwa kushtukiza lakini akaitika na amekuja ametufanyia jambo. Tunamshukuru sana kwa mchango wake na ni jambo tumemshtukiza abarikiwe sana" Amesisitiza



Kwa upande wake, ofisa Maendeleo ya jamii wa Kata ya Bugarama, Anna Mwakalinga, amewahimiza wanawake kuachana na mikopo umiza, badala yake waanzishe vikundi vya ushirika ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.


Mwakalinga ambaye awali alikuwa ofisa maendeleo wa kata ya Bulyanhulu kilipo kikundi hicho, amesema kwa sasa wanaendelea na taratibu za kuwaelimisha wanakikundi hao ili waweze kunufaika na fursa ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri kwenda kwa akina mama, vijana na wenye ulemavu. 


"Ni kweli Halmashauri yetu ya Msalala tunazo fedha kwa ajili ya kuwaendeleza akina mama, vijana na wenye ulemavu, lakini  kikundi hiki ni moja ya vikundi vilivyopo kata ya Bulyanhulu" Amesema Mwakalinga


"Kulingana na lengo la uanzishwaji wa kikundi hiki la kusaidiana katika shida na raha, hakikuwa kimekidhi vigezo vya kunufaika na mikopo hii kutokana na hawakuwa na mradi wa pamoja, ila tunaendelea kuwaelimisha na watakapotimiza vigezo watanufaika kwa sababu ndilo lengo la serikali yetu" Ameongeza


Hata hivyo Mwakalinga amewapongeza na kuwashukuru wadau waliojitokeza kwa ajili ya kuwashika mkono akina mama wa kikundi hicho ili kiweze kuwa na mradi wa pamoja na kuendelea kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo.


Kikundi cha Super Women kinatambulika kama kikundi cha kusaidiana nyakati za shida na raha, kina zaidi ya wajumbe 110, huku serikali kupitia kwa afisa maendeleo ya jamii wa kata hiyo na kata jirani wakikiandaa kikundi hicho pamoja na vingine kwa ajili ya kunufaika na mikopo hiyo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri ya Msalala.


Hata hivyo, kikundi hicho kinaendeshwa kwa kauli mbiu yenye msukumo mkubwa wa kijamii, kwa lengo la kuwaleta pamoja wanawake wa Kakola kuweza kusaidiana na kuinuana.


"UPENDO NA MSHIKAMANO KATIKA KUSAIDIANA KWENYE SHIDA NA RAHA, PAMOJA TUNAWEZA KUINUA UCHUMI"

TAZAMA PICHA 👇
Mgeni rasmi katika hafla hiyo Matani Kishepo (kulia) akiongoza zoezi la kukata keki pamoja na mwenyekiti wa kikundi cha Super Women kilichopo Kakola halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.


Mwisho.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso