MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO HALMASHAURI YA USHETU. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 27 July 2025

MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO HALMASHAURI YA USHETU.



Na. Emmanuel Shomary, Ushetu


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, ameendelea na ziara yake ya kikazi katika wilaya za Mkoa huo kwa lengo la kujionea hatua ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo Julai 26, 2025, ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa katika kusimamia Miradi inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja.


Katika ziara hiyo, Mhe. Mhita ametembelea miradi kadhaa ikiwemo Ujenzi wa Shule ya Msingi Igwamanoni kata ya Igwamanoni inayolenga kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto.

Aidha, alikagua ujenzi wa mashine ya kuchakata mazao ya kilimo uliopo kata ya Bulungwa, ikiwa ni hatua ya kuwawezesha wakulima kuongeza thamani ya mazao yao na kukuza uchumi wa kaya.


Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa alitembelea Kituo cha Afya Bulugwa ambako ujenzi wa wodi ya wazazi unaendelea. Mradi huo unatarajiwa kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto kwa kupunguza umbali wa kufuata huduma hizo.


Miradi mingine ni pamoja na upandaji miti uliopo shule ya msingi Butibu, kata ya Kinamapula, kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira.


Pia alikagua ujenzi wa tenki kubwa la maji na mtandao wa usambazaji maji safi na salama katika maeneo ya vijijini, uliopo kata ya Bukomela pamoja na ujenzi wa shule mpya ya Amali iliyopo kata ya Nyamilangano ambayo itasaidia kuwapa vijana elimu ya ufundi na kuwajengea uwezo wa kujiajiri.


Akizungumza baada ya kutembelea miradi hiyo, Mhe. Mhita amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, usimamizi wake na jinsi inavyolenga kuboresha maisha ya wananchi. Amewapongeza viongozi na watendaji wa halmashauri ya Ushetu kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango na ndani ya muda.


“Mkoa wa Shinyanga una fursa kubwa ya maendeleo, ni wajibu wetu wote kuhakikisha tunazitumia kikamilifu. Halmashauri ya Ushetu imeonyesha mfano mzuri kwa usimamizi wa miradi, tunataka kuona kila halmashauri inakwenda kwa kasi hii,” amesema Mhe. Mhita.


Ziara ya mkuu huyo wa mkoa ni sehemu ya utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhimiza uwajibikaji kwa watendaji wa serikali ili kufanikisha ajenda ya maendeleo ya Taifa.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso