Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Prof. Peter Msoffe amesema miradi ya nishati safi ina umuhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi yanayotokana na ukataji wa miti.
Amesema hayo wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Jiko la Mfano (model cooking school Kitchen) katika Shule ya Msingi Kibasila mkoani Dar es Salaam ikiwa ni hatua za utekelezaji wa Mradi wa Kuongeza Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Mashuleni Nchini.
Amesema mradi huo utakaowezesha wanafunzi 640 kupikiwa chakula, si tu utasaidia kuokoa muda wa kuandaa chakula lakini pia utalinda mazingira na afya za wapishi kwa kuwa majiko hayo yanayotumia umeme hayazalishi hewa chafu.
Aidha, Naibu Mkuu Prof. Msoffe alitoa wito kwa uongozi wa shule hiyo kuhakikisha miundombinu hiyo inalindwa na kutunzwa ili taasisi zingine zijufunze kupitia jiko hilo la mfano.
Kutokana na jitihada hizo alitoa pongezi kwa wadau hao wa maendeleo ambao ni Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na SEforALL pamoja na Serikali ya Uingereza kwa kufanikisha mradi huo.
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Bi.Marianne Young amepongeza jitihada zinazotekelezwa Serikali ya Tanzania katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuweka mazingira wezeshi.
Pia, Balozi huyo alisema kuwa Serikali ya Uingereza itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano kutoka Taasisi ya SEforALL Bw. Mikael Melin alipongeza Serikali na sekta binafsi kwa ushirikiano wao tangu mwanzo wa maandalizi ya utekelezaji wa mradi huo hadi kufikia sasa.
Akitoa shukrani, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kibasila Bi. Halima amepongeza wadau wote kwa kuchagua shule hiyo kuwa ya kwanza na ya mfano katika utekelezaji wa mradi.
Pamoja na hayo, Bi. Halima aliahidi kuwa uongozi wa shule hiyo utalinda na kutunza miundombinu hiyo ili kuhakikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha lengo la matumizi ya nishati safi linafikiwa. Ofisi ya Makamu wa Rais
No comments:
Post a Comment