WANNE WACHOMWA MOTO KAHAMA: POLISI WALANI KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 17 June 2025

WANNE WACHOMWA MOTO KAHAMA: POLISI WALANI KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI

NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha tukio la kusikitisha lililotokea alfajiri ya leo Juni 17, 2025, katika Mtaa wa Mhongolo, Manispaa ya Kahama, ambapo watu wanne wanaodhaniwa kuwa ni vibaka wameuawa kwa kupigwa mawe na kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.


Kamanda Magomi amelaani vikali tukio hilo na kusisitiza kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kujichukulia sheria mkononi, akibainisha kuwa uchunguzi mkali umeanza huku msako wa kuwatafuta waliohusika ukiendelea.


Kwa mujibu wa mashuhuda, Ibrahimu Jacob, mkazi wa Mhongolo amesema eneo hilo limegeuka kuwa hatari hasa nyakati za usiku ambapo watu huvamiwa na kuporwa mali zao.


Ibrahimu amesema yeye mwenyewe ameshawahi kupigwa na kuporwa zaidi ya mara moja ambapo ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuongeza doria na kusisitiza kuwa baadhi ya vibaka hujificha kwenye maeneo ya miembe karibu na shule.


Mmoja wa waliojeruhiwa kwa kukatwa panga kichwani usiku wa kuamkia leo Stephano Maganga amesema ameshambuliwa baada ya kwenda kufuatilia simu ya mdogo wake ambayo aliyonyang'anywa na vijana wakati akienda kwenye harusi saa 5 usiku wa kuamkia leo.


Stephano ameeleza kuwa alipofika kwa vijana hao ambao wanasadikika kuwa ni vibaka na kuwauliza kuhusu simu ya mdogo wake ndipo walimshambulia kwa kumpiga mabapa ya panga na alipojaribu kujitetea wakafanikiwa kumkata panga kichwani.


Katika mahojiano, Juma Benard, mkazi mwingine wa Mhongolo, amesema tatizo hilo linasababishwa na vijana wengi kushinda vijiweni badala ya kufanya kazi halali na ameeleza kuwa baadhi yao hujifanya wateja wa bodaboda halafu wanawavamia waendesha pikipiki na kuwapora pia amesema tukio hili liwe funzo kwa vijana wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu.


Mwenyekiti wa mtaa wa Mhongolo, Emanuel Nangale, amesema alipokea taarifa za tukio hilo mapema asubuhi na alifika eneo la tukio akiwa na viongozi wenzake, Wakati huo tayari wananchi walikuwa wamechukua sheria mikononi kwa kuwaua vijana hao.


Nangale ameeleza kuwa kwa mujibu wa taarifa alizozipata, kuna mama aliyeporwa alfajiri ya leo wakati akielekea kwenye maombi ya asubuhi kanisani na mwanae kujeruhiwa wakati wa purukushani hiyo.


Kwa upande wa Jeshi la Polisi, Kamanda Magomi amesema kuwa bado miili ya vijana hao haijatambuliwa na amesisitiza kuwa hata kama mtu anatuhumiwa kwa uhalifu, sheria ndiyo njia sahihi ya kushughulika naye huku akionya kuwa tabia ya kujichukulia sheria mkononi iachwe.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso