Kwa mwaka wa pili mfululizo Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama, Mkoani Shinyanga, imepata hati safi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Akizungumza katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwa ajili ya kujadili taarifa ya hoja na mpango kazi wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG kuhusu hesabu za mwaka wa fedha 2023/2024, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Bi. Mboni Mhita, ameipongeza Halmashauri kwa mafanikio hayo.
Bi. Mboni amewataka madiwani kuendeleza ushirikiano wao na wataalamu wa Halmashauri uliochangia mafanikio hayo, sambamba na kuimarisha usimamizi wa mapato kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Ushetu.
Aidha, ameshauri Halmashauri kuhakikisha inakamilisha taratibu za upatikanaji wa hati miliki ya eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri hiyo, ili kuepusha migogoro na wananchi wasiowaaminifu wanaodai kumiliki maeneo ya serikali.
“Serikali imeleta fedha nyingi sana kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya utawala. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesisitiza kila Halmashauri kuwa na jengo la kisasa, Haitakuwa busara mabilioni ya fedha kuelekezwa kwenye eneo ambalo bado halina hati miliki,” amesema Bi. Mboni.
Akaongeza:
“Ni muhimu kukamilisha taratibu zote za kisheria ili kuzuia mvutano wa umiliki, kwani kuna watu wenye nia ovu wanaoweza kudai eneo ni lao.”
Kuhusu utekelezaji wa miradi, amewakumbusha watendaji wa Halmashauri kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati, badala ya kusubiri hadi mwisho wa mwaka wa fedha ambapo fedha hurudishwa serikalini huku wananchi wakihitaji huduma hizo.
“Kama tukipewa fedha kwa ajili ya mradi fulani halafu zikarudi, ina maana hatuko tayari kuutekeleza, Tuyaishi mapenzi ya Rais wetu kwa wananchi wake na tusimwangushe,” amesisitiza.
Pia amewataka watendaji kufanyia kazi mapendekezo ya CAG na kuhakikisha hoja zilizobaki zinapatiwa majibu kwa wakati.
Mikopo na Ustawi wa Wananchi
Akizungumzia maendeleo ya wananchi, Bi. Mboni amewahimiza wakazi wa Kahama kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ikiwemo asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.
Amewaagiza maafisa wanaohusika na utoaji wa mikopo hiyo kufuatilia kwa karibu urejeshaji wa mikopo ili kuwasaidia wananchi wengine wanaohitaji huduma hiyo.
“Mheshimiwa Rais hataki kuona wananchi wananung’unika au kukata tamaa, Njia bora ya kumshukuru ni kuunga mkono juhudi zake, kumuombea na kuwahamasisha wananchi kuchangamkia mikopo hizi,” amesema.
Kauli za Viongozi wa Halmashauri
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Mheshimiwa Gagi Lala, amesema mafanikio hayo yametokana na mshikamano baina ya madiwani, ofisi ya Mbunge na wakuu wa idara katika ofisi ya Mkurugenzi.
“Umoja wetu ndio silaha kubwa iliyotuvusha hadi kufikia hatua hii. Tunaamini tutaendelea kufanya vizuri zaidi,” amesema Gagi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi. Essery Pima, ameeleza kuwa tayari wameandaa mpango kazi wa kushughulikia mapendekezo yote ya CAG na kuwagawia wakuu wa idara majukumu mahsusi ya kushughulikia hoja zilizobaki ndani ya muda uliopangwa.
“Tumejipanga kuhakikisha hoja zote zinapatiwa majibu kwa wakati, na kwa mwaka 2024/2025 tunaamini tutazidi kuboresha zaidi,” amesema Essery.
Maelekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Shinyanga, CPA Yusuph Mambwe, amesema baadhi ya hoja zilizotolewa na CAG tayari zimefanyiwa kazi huku zingine zikiwa kwenye hatua za utekelezaji.
“Kaguzi zimefanywa kwa mujibu wa Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha 10 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma, Sura ya 418. Tunatarajia Halmashauri kuwasilisha vielelezo baada ya utekelezaji kukamilika,” amesema.
Mwito kwa Halmashauri
Diwani wa Kata ya Kinamapula, Mheshimiwa Sharif Samwel, ameiomba Halmashauri kuendeleza juhudi nzuri zinazofanyika kwa sasa ili Ushetu iendelee kuwa na hati safi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment