EZEKIEL MAIGE AREJEA TENA: ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA MSALALA KWA TIKETI YA CCM - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 28 June 2025

EZEKIEL MAIGE AREJEA TENA: ACHUKUA FOMU YA UBUNGE JIMBO LA MSALALA KWA TIKETI YA CCM





NA NEEMA NKUMBI - HUHESO DIGITAL KAHAMA



Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Msalala na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, mstaafu Ezekiel Maige, leo Juni 28, 2025 amechukua rasmi fomu ya kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), akieleza kuwa ameitikia wito wa wananchi zaidi ya 23,000 waliomtaka kurejea kwenye ulingo wa siasa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Maige amesema kuwa amekuwa akipokea simu na ujumbe kutoka kwa wananchi wake kwa kipindi cha mwaka mmoja, wakimtaka arudi kuongoza jimbo hilo.


“Zaidi ya wananchi elfu 23 wamekuwa wakinipigia simu kwa kipindi cha mwaka mmoja, wakiniuliza kama nagombea au la, Nilikuwa nikiwaambia kuwa nitasema muda ukifika Ndio maana leo nimeamua kuzungumza nanyi ili kuwaambia kuwa tayari nimeshachukua fomu,” amesema Maige.

Mbali na mwitikio huo wa wananchi, Maige amesema amesukumwa pia na kiu ya mabadiliko katika Jimbo la Msalala, hasa kutokana na hali ya sasa ya mahusiano duni kati ya viongozi na wananchi.


“Kwa miaka mitano iliyopita kumekuwa na changamoto kubwa za kimahusiano kati ya viongozi na wananchi Hali hiyo imepunguza kasi ya maendeleo na kuondoa mshikamano hivyo Mimi ninarejea kuleta umoja na kasi mpya ya maendeleo,” ameongeza.

Amebainisha pia kuwa mojawapo ya sababu nyingine iliyomfanya arejee katika siasa ni kuondoa upotoshaji kuhusu baadhi ya miradi aliyoianzisha wakati akiwa mbunge na waziri, ametolea mfano wa ujenzi wa barabara ya Geita–Bukoli–Kahama yenye urefu wa kilomita 107, akisema kuwa mchakato wa barabara hiyo ulianza akiwa bado madarakani kupitia ilani ya CCM ya mwaka 2010–2015, kifungu cha 64 kipengele (e), na kuendelezwa katika ilani ya 2015–2020 kifungu cha 39 kipengele (d).


“Kiongozi aliyenifuata alichokifanya ni kuendeleza kile nilichokianzisha, Si kweli kwamba barabara hii ilianzishwa baada yangu,” amesema Maige.

Hatua hii ya Maige inakuja wakati ambapo CCM inaendelea na mchakato wa ndani wa kuchukua na kurejesha fomu za uteuzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Ezekiel Maige, ambaye aliwahi kuhudumu katika serikali ya awamu ya nne, alijizolea umaarufu kutokana na misimamo yake kuhusu uhifadhi wa rasilimali za taifa pamoja na juhudi za kupeleka maendeleo kwa wananchi wa Msalala.

Kauli mbiu yake kwa safari hii ni: “UKOMBOZI WA MSALALA NI SASA.”

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso