SERIKALI YA MTAA WA NYAKATO YA MALIZA MGOGORO ULIODUMU MIAKA 25 SOKO LA MAGWANJI KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday 15 May 2024

SERIKALI YA MTAA WA NYAKATO YA MALIZA MGOGORO ULIODUMU MIAKA 25 SOKO LA MAGWANJI KAHAMA





NA NEEMA NKUMBI HUHESO DIGITAL& HUHESO FM-KAHAMA

Wakazi wa mtaa wa Nyakato, kata ya Nyasubi katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanya, wameishukuru serikali ya mtaa huo, kwa kuumaliza mgogoro wa soko la Magwanji uliodumu kwa Zaidi ya miaka 25 sasa, uliokuwa ukikwamisha kuanza kwa shughuli za soko, sambamba na kuchelewesha maendeleo ya mtaa huo.

Wakazi hao ambao ni wajasiriamali, Lulu Shigongo na Flora Peter, wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa hafla ya uzinduzi rasmi wa soko hilo, wamewaomba viongozi wa ngazi za kata, vijiji na mitaa, kutoingiza tofauti zao za kisiasa katika miradi ya maendeleo, kwani kufanya hivyo ni kukwamisha maendeleo ya maeneo husika, na kwamba uwepo wa soko hilo utawanufaisha wao binafsi pamoja na kuchangia maendeleo ya mtaa wa Nyakato.

“Ni soko ambalo nalitegemea litakuwa ni kubwa na watu wengi, kwa hiyo pia nimeona nitoke kule nije huku ili pia nipunguze gharamaya nauli, maana mwanzo kwenda kule soko kubwa nilitumia nauli shilingi 2000 kwa siku, lakini hapa sitakuwa na nauli yoyote nitatembea tu, kwa hiyo naishukuru sana serikali” Alisema Flora

Hussein Mwita ni mwenyekiti wa mtaa wa Nyakato aliwataka wajasiriamali waliopata maeneo katika soko hilo, kuyatumia kama ilivyo makubaliano vinginevyo watapokonywa na kugawiwa kwa watu wengine.

“Kwa nyinyi ambao mmebahatika kupata eneo la kibanda, mlitumie kama tulivyokubaliana, kwa sababu ukiliachaniza, wahitaji ni wengi tutaona namna ya kufanya” Alisema Mwita

Mola Zablon ni msemaji wa chama cha mapinduzi – CCM kata ya Nyasubi manispaa ya Kahama, amewarai viongozi wa machinga wilaya ya Kahama, kusimamia maadili kwa wanachama wao, huku makamu mwenyekiti wa soko la Magwanji Bakari Fundikira, akieleza mwitikio wa watu kuwekeza katika soko hilo

“Lakini siku moja nilikuja huku, kuna watu wako humu, yaani mtu anataka eneo, anapewa halafu anatafuta mtu anamuuzia, mtu wa namna hiyo ukimuona mnyang’anye eneo mpe masikini kabisa wa mwisho bure, afanye kazi apate mtaji, haiwezekani wewe unapewa bure halafu unageuka kuwa dalali hapana” Alisema Mola

“Na hili niliseme mbele ya viongozi wa machinga, ndugu zangu umepewa eneo bure, hatutarajii kuona mkandarasi mwingine amekuja hapa amenunua kwa gharama, vinginevyo umoja wenu hautakuwa ni umoja tunaoutaka hapa, utakuwa ni uvurugaji, tunahitaji tuwape maeneo bure, mfanye biashara hapa mpate pesa, mpeleke Watoto shule, lakini na sisi mtuhudumie wananchi wetu hapa” Aliongeza Mola



Soko la Magwanji lililokuwa na mvutano wa takriban miaka 25, unaotajwa kukwamisha shughuli za soko pamoja na maendeleo ya mtaa wa Nyakato, limezinduliwa rasmi kuanza shughuli zake, linatarajiwa kuwa na wafanyabiashara ndogondgo (machinga) Zaidi ya 300, linatajwa pia kupunguza changamoto ya ajira kwa vijana sambamba na kupunguza uhalifu mdogomdogo unaodaiwa kufanywa na baadhi ya vijana wanaoshinda vijiweni bila kazi maalum.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso