MCHENGERWA AIPA DART MIEZ SABA KUPATA MWEKEZAJI BINAFSI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday 19 March 2024

MCHENGERWA AIPA DART MIEZ SABA KUPATA MWEKEZAJI BINAFSI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohammed Mchengerwa ameielekeza Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (DART) kufikia Oktoba 2024 iwe imempata mwekezaji binafsi ambaye ni mtoa huduma wa mabasi hayo ili kuleta ufanisi.



Mchengerwa ametoa maelekezo hayo jana Machi 18, 2024 wakati akiwasilisha Randama ya Bajeti ya Ofisi ya Rais Tamisemi Fungu namba 56 na namba 2 la Tume ya Utumishi wa Walimu mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, katika ukumbi wa Anne Makinda uliopo bungeni jijini Dodoma.

“Nilishawaambia watu wa Dart wakati wanakuja kunipitisha kwenye mfumo tunaokwenda nao ikifika Oktoba wakishindwa kuhakikisha wanampata mwekezaji atakayekwenda kuhudumia njia hii wa sekta binafsi na kushindwa kuhakikisha mabasi yamepatikana waniletee barua za kujiuzulu, na tumeshakubaliana na hakuna mjadala watu wanataka huduma,” amesema Mchengerwa.

Mchengerwa amesema kuwepo kwa mwekezaji binafsi mradi huo utaendeshwa kwa ufanisi kutokana na kulipa kodi kwa Serikali, na wakati huohuo atawajibika endapo atatoa huduma isiyostahili.

“Atahakikisha anatoa huduma nzuri ili kama tukileta mabasi ya kutosha watu wa Dar es Salaam wataegesha magari yao watatumia mwendokasi na tutakwenda kuokoa zaidi ya Sh300 bilioni ambayo tungeitumia kununua mabasi,” amesema Mchengerwa.

Waziri huyo ameongeza kuwa ifikapo Septemba hadi Oktoba Serikali itakuwa imepata mabasi ya kutosha ya kuendesha njia zote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo sekta binafsi ili Watanzania wa Dar es Salaam wahudumiwe vizuri kabla ya kuanza kupeleka huduma ya mwendokasi kwenye majiji mengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Denis Londo amepongeza uamuzi huo na kusema kuwa maamuzi hayo yataacha alama nzuri kwa waziri aliyekuwepo kutokana na kuwa mbunifu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso