MADHEHEBU MBALIMBALI YA DINI YAKUSANYIKA SHINYANGA KUMUOMBEA DUA NA SALA RAIS MSTAAFU HAYATI ALI HASSAN MWINYI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday 4 March 2024

MADHEHEBU MBALIMBALI YA DINI YAKUSANYIKA SHINYANGA KUMUOMBEA DUA NA SALA RAIS MSTAAFU HAYATI ALI HASSAN MWINYI

 

WANANCHI kutoka Madhehebu Mbalimbali ya kidini mkoani Shinyanga, wamemuombea Dua na Sala Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili nchini Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi apumzike kwa Amani.



Na Marco Maduhu,SHINYANGA


Maombi hayo yamefanyika leo Machi 4 kwenye Viwanja vya Sabasaba Manispaa ya Shinyanga huku Mgeni Rasmi akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.


Akizungumza kwenye maombi hayo, Mndeme kwanza amewashukuru wananchi wa Shinyanga kutoka Madhehebu mbalimbali kujitokeza kumuombea Rais Mstaafu Hayati Ali Hassan Mwinyi apumzike kwa Amani, na kuahidi kwamba watayaenzi yale mema ambayo amewaachia.


“Tumekusanyika hapa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kutoka Madhehebu mbalimbali ili tumuombee Dua na Sala Rais wetu Mstaafu Hayati Ali Hassan Mwinyi ili Mwenyezi Mungu ampokee katika Ufalme wake na ampatie pumziko la Amani,”amesema Mndeme.


“Tumuombee pia Rais Wetu Samia Suluhu Hassan kwa Msiba huu Mzito ambao ameupata kwa kuondokewa na kiongozi Mkubwa ambaye alikuwa akimtegemea pia katika ushauri mbalimbali namna ya kuongoza nchi na kuwatumikia Watanzania,”ameongeza Mndeme.


Aidha, aliitakia pia pole Familia yote ya Marehemu Hayati Ali Hassan Mwinyi pamoja na Wajane ambao wameachwa kwamba Mwenyezi Mungu awapatie faraja katika kipindi hiki kigumu ambacho wameondokewa na mpendwa wao.
Katika hatua nyingine Mdeme, amewakaribisha Wananchi wa Shinyanga na viongozi mbalimbali, kwamba wafike kwenye Ofisi za Mkoa huo Kusaini Kitabu cha Maombolezo


Naye Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga Ismail Makusanya, akizungumza kwenye Maombi hayo, amesema katika Mkoa huo hawatamsahau Rais Mwinyi kwa kutatua mgogoro mkubwa ambao ulikuwepo wa kiimani, ambapo aliutatua na kudumisha amani.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili nchini Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi alifariki dunia Februari 29 mwaka huu akiwa na miaka 98 alipokuwa akipatiwa Matibabu katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam na amezikwa Machi 2, 2024 huko Unguja, Zanzibar.


Alikuwa Rais wa Pili wa Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995, Bwana ametoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe Amina.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso