TUONGEZE NGUVU KWA PAMOJA KATIKA KUPAMBANA NA JANGA LA UKIMWI - WAZIRI SHAMATA SHAAME - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday 7 August 2023

TUONGEZE NGUVU KWA PAMOJA KATIKA KUPAMBANA NA JANGA LA UKIMWI - WAZIRI SHAMATA SHAAME

Mratibu kutoka Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Mathew Mwinuka akitoa maelezo kwa Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis kuhusu shughuli zinazotekelezwa na programu hiyo wakati wa maonesho ya Nane nane yanayoendelea Jijini Mbeya
.

Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Dkt. Henry Kissinga akitoa maelezo kwa Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis kuhusu masuala ya Afya Moja walipotembelea katika banda la Ofisi hiyo katika maonesho ya Nane nane yanayoendelea Jijini Mbeya.

Picha ya Pamoja ya baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) walioshiriki katika maonesho ya Nane Nane katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Picha ya Pamoja ya baadhi ya watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) walioshiriki katika maonesho ya Nane Nane katika viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.


NA. MWANDISHI WETU - MBEYA


Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar Mhe. Shamata Shaame Khamis amehimiza wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika Mapambano Dhidi ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa kuhusu masuala hayo.


Ametoa rai hiyo Agosti 6, 2023 alipotembelea Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu katika maonesho ya Kilimo Kimataifa yanayoendeleo Jijini Mbeya. Maonesho ya mwaka huu yamebebwa na Kauli mbiu inayosema “Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa mifumo Endelevu ya Chakula”


“Tunapaswa kuungana kwa pamoja, katika mapambano haya ya Virusi vya UKIMWI na kuhakikisha kila anayegundulika na maambukizi kuzingatia matumizi sahihi ya dawa, kujilinda na kulinda wengine,” alisema Mhe. Shamata


Alitumia nafasi hiyo kukemea masuala ya unyanyapaa na kuhimiza jamii kuchukuliana na kuungana pamoja kupambana na maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI.


Akizungumzia kuhusu masuala ya maafa nchini Waziri Shamata aliikumbusha jamii kuzingatia taarifa za utabili wa hali ya hewa zinzotolewa na Mamalaka yua Hali ya hewa kwa lengo la kuchukua tahadhali dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza na kujikinga na maafa.


“Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inailinda jamii yake katika majanga mbalimbali, ili kuendelea kuishi kwa furaha na usalama bila kukubwa na madhara yatokanayo na maafa nchini.


Naye Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Menejimenti ya Maafa anayeshughulikia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Prudence Constantine akizungumza na waandishi wa habari alieleza kuwa, Ofisi imeendelea kutoa elimu kwa umma katika maonesho hayo juu ya uelewa wa matumizi sahihi ya bendera ya Taifa, kujua Nembo sahihi ya Serikali, pamoja na shughuli za uchapaji wa nyaraka na majukumu ya Baraza la Taifa la Biashara nchini.


“Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu yenye jukumu la kuratibu shughuli za Serikali na katika maonesho haya ya Kimataifa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi maarufu kama Nane Nane imeshiriki kwa kuhusisha baadhi ya Idara zake na taasisi ikiwemo,Idara ya Menejimenti ya Maafa, Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Nchini (TACAIDS), Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa lengo la kutoa elimu kwa umma,”alieleza prudence.


Aidha alieleza kuwa elimu zaidi itaendelea kutolewa katika masuala ya menejimenti ya maafa kuanzia ngazi ya Kijiji hadi Mkoa ili kuwajengea uwezo kukabiliana na maafa nchini.


Aidha kuhusu Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) alibainisha kuwa itaendelea kuratibiwa vizuri kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuimarisha na kuboresha utekelezaji wa programu hiyo.


“Ninakushukuru Waziri wa Kilimo Zanzibar Mhe. Shamata kwa kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu na kukiri kuridhishwa na huduma zinazotolewa hapa, tunaahidi kuendelea kutoa elimu kwa umma ili jamii iwe na uelewa wa pamoja juu ya shughuli za uratibu wa Serikali,”alisema Prudence

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso