MWANAMKE APIGWA MATEKE TUMBONI NA MUMEWE NA KUFARIKI JAMAA AFUNGWA JELA MIAKA NANE-MWANZA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday 1 August 2022

MWANAMKE APIGWA MATEKE TUMBONI NA MUMEWE NA KUFARIKI JAMAA AFUNGWA JELA MIAKA NANE-MWANZA



MAHAKAMA Kuu Tanzania Kanda ya Mwanza, imemhukumu Bahati Marko (45), kifungo cha miaka minane jela kwa kosa la kumuua mkewe, Esta Josefu kwa kumpiga mateke tumboni na kufariki dunia papo hapo. 


Mwanamke huyo ameacha mtoto mchanga wa siku saba. 


Kabla ya hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, John Kahyoza, Wakili wa Serikali, James Pallangio, akimsomea mshtakiwa maelezo ya kesi yake, alisema mwanaume huyo alimtaka mkewe aliyekuwa amejifungua kwenda kuishi kwa mama yake, lakini mke alikataa ndipo ugomvi upolizuka na kumpiga hadi kifo. 


Wakili Pallangio alidai tukio hilo lilitokea Januari 28, mwaka 2020 na kwamba mshtakiwa na mke wake walikuwa wakiishi katika kijiji cha Shilabela/Lulembela, Wilaya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita. 


Alidai, baada ya mshtakiwa huyo kugundua kuwa mke wake amefariki aliondoka kwenda mgodini na kukaa hadi alipokamatwa na polisi na kupelekwa kituo cha Masumbwe, baada ya mahojiano alifikishwa mahakamani. 


Baada ya maelezo ya awali, Jaji Kahyoza alimuuliza mshtakiwa huyo kama maelezo aliyosomewa na wakili yana ukweli. Mshtakiwa huyo alijibu, “ni kweli nilimuua mke wangu bila kukusudia.”


Jaji Kahyoza alimuuliza mshtakiwa alitumia nini kumuua mke wake na kujibu alitumia mikono yake kwa kumpiga mateke tumboni na ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake na kufariki dunia papo hapo na kuondoka kwenda mgodini.


Kutokana na mshtakiwa kukiri kosa lake, Jaji Kahyoza alimsomea hukumu hiyo. “Mahakama hii imekutia hatiani kwa kukiri kosa lako la kumuua mke wako bila kukusudia, pia mahakama hii inakutaka ujitetee ili iweze kukupunguzia adhabu.” 


Mshtakiwa huyo akitetewa na wakili wa kujitegemea Penina Mashimba, alidai kuwa mteja wake amejutia ndiyo maana amekiri kosa bila ya kulazimishwa. 


Aidha, alidai mteja wake amekaa mahabusu miaka miwili na miezi sita na amejifunza na kuiomba mahakama hiyo kumpa adhabu ndogo ya kifungo cha nje. 


Wakili Pallangio aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kwa kuwa inaonyesha mshtakiwa huyo hakutumia busara katika kumwadhibu mkewe hasa sababu iliyotolewa na kwamba alikuwa na mfumo dume.


Alidai mtuhumiwa huyo hata baada ya kumpiga alimuacha na kuondoka kwenda mgodini hadi hapo polisi walipomkamata.


“Alimpiga mchana tena akiwa ana mtoto mchanga wa siku saba na kusababisha mtoto kukosa mapenzi ya mama yake, hivyo naomba mahakama hii itowe adhabu kali kwa mshtakiwa, ili iwe fundisho kwa wanaume wenye tabia ya kuwapiga wake zao,” alisema. 


Jaji Kahyoza alisema kosa alilolitenda mshtakiwa linastahili kifungo cha maisha, na kwamba tukio hilo ni la kikatili na kumhukumu jela miaka minane.

Chanzo:Nipashe

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso