WANAWAKE WATANO WAUAWA NA KUNYOFOLEWA SEHEMU ZA SIRI MTWARA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 13 May 2022

WANAWAKE WATANO WAUAWA NA KUNYOFOLEWA SEHEMU ZA SIRI MTWARA



Wanawake watano wilayani Masasi mkoani Mtwara wameuawa kikatili na watu wasiojulikana huku watatu kati yao wakikutwa sehemu zao za siri zimenyofolewa. 


Mauaji hayo yamefanyika katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, hatua ambayo imesababisha wananchi kuingiwa na hofu juu ya usalama wao. 


Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Claudia Kitta amesema amesikitishwa na mauaji hayo ambayo yameonyesha taswira mbaya hasa kutokana na wanawake kuuawa na kunyofolewa viungo vyao.


“Inasikitisha kuona kwamba ndani ya miezi mitatu, wanawake watano wamekutwa wameuawa katika maeneo tofauti. Hali hii inasikitisha na inatishia usalama wa wananchi,” alisema Kitta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya. 


Amesema jambo ambalo linashangaza ni kwamba aina ya mauaji ni moja huku sababu zikiwa hazijafahamika na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi bado linaendelea na uchunguzi Kutokana na mauaji hayo.


Kitta amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya inaendelea kuimarisha ulinzi ikiwa ni pamoja na kulinda mali za wananchi na kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa. 


Kitta amewataka wananchi wilayani humo kushirikiana na polisi kuhakikisha wahusika wa matukio hayo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. 


Amesema njia ya peke ambayo pia inaweza kutumika katika kuimarisha ulinzi na usalama ni kuanzisha ulinzi shirikishi ngazi za kata, vijiji na mitaa hatua ambayo alisema itasaidia kupunguza matukio ya mauaji yanayoendelea wilayani hapa.


Pia amewataka wananchi kutoa taarifa polisi pale wanapowaona watu ambao hawawafahamu kwenye maeneo yao ili wafuatiliwe na kujua uhalisia wake. 


Baadhi ya wananchi waliozungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti walisema vitendo hivyo vimesababisha hofu miongoni mwa wananchi hasa kinamama ambao mara kwa mara wamekuwa wakijishughulisha na uzalishaji mali wanaotoka nyumbani na kwenda kwenye shughuli zao na kurudi. 

CHANZO:NIPASHE

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso