RC TELACK ASISITIZA UTOAJI TAARIFA MATUKIO YA UKATILI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday 12 February 2021

RC TELACK ASISITIZA UTOAJI TAARIFA MATUKIO YA UKATILI

 

Asasi ya kiraia ya wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga, ambayo inajishughulisha na kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, pamoja na kupambana na umaskini imezinduliwa rasmi leo.

PICHA: Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akizungumza kwenye uzinduzi wa Asasi ya Wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga.

 

Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, na kuhudhuriwa na wanawake mkoani Shinyanga, Asasi za kiraia, Taasisi za kifedha, Hakimu, Ofisa maendeleo, viongozi wa CCM, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack.

 

 Akisoma Risala kwa mgeni rasmi,Katibu wa Asasi ya wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga Pendo Sawa, amesema lengo la asasi hiyo ni kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake, pamoja na kujengeana uwezo wa kuinuana kiuchumi.

 

PICHA: Meneja Biashara kutoka Benki ya CRDB Mwanahamisi Iddi, akielezea fursa za wanawake zilizopo kwenye Benki hiyo.

Amesema Asasi hiyo ilianzishwa Mwaka 2020, na sasa imezinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya kuendeleza mapambano ya kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, vikiwemo vipigo, ubakaji, kulawiti, kutekeleza familia zikiwemo mimba na ndoa za utotoni.

 

“Changamoto ambayo tumeiona sisi Asasi ya Wanawake Laki Moja juu ya kuendelea kwa matukio ya ukatili mkoani Shinyanga dhidi ya wanawake na watoto, ni tatizo la mila na desturi kandamizi, ambazo zimekuwa mwiba kwa jinsi ya kike na kuendelea kunyanyasika ndani ya jamii,”amesema Sawa.


“Kutokana na changamoto hii ya kuendelea kwa matukio ya ukatili mkoani Shinyanga, tunaomba Serikali ishirikiane na asasi za kiraia kutoa elimu kwa wananchi namna ya kupambana na matukio ya ukatili ndani ya jamii, ikiwamo na kuzijua sheria ya kupigania haki zao hasa kwa wanawake wajane ambao wamekuwa wakidhulumiwa mali wanapofiwa na waume zao,”ameongeza.

 

Naye Mwenyekiti wa wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga Annaskolastika Ndagiwe, ameeleza kusikitishwa na matukio ya ukatili ambayo yanaendelea kutendeka mkoani Shinyanga, huku wahusika wa matukio hayo wakishindwa kuchukuliwa hatua stahiki, na kuendelea kuishi Uraiani kitendo ambacho amebainisha kinaumiza sana.

 

Amesema kuna baadhi ya matukio ameshayatolewa taarifa kwenye mamlaka husika juu ya tukio la watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili, lakini cha ajabu wahusika wa matukio hayo hakuna hatua zozote za kisheria ambazo zimechukuliwa juu yao, jambo ambalo linawapa ugumu katika kuendeleza mapambano ya kupinga ukatili ndani ya jamii.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, amewapongeza katika kuendeleza mapambano ya kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto, pamoja na kuinuana kiuchumi.

 

Amesema Asasi hiyo ipo katika muda muafaka, ambapo Mkoa huo unapambana na kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, na kuwataka wanawake hao watoe taarifa za matukio ambayo wanafanyiwa watoto wao, pamoja na wao wenyewe, ili wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria na kumaliza vitendo hivyo vya ukatili ndani ya jamii.

 

Telack amesema baadhi ya wanawake wamekuwa hawatoi taarifa za matukio ya ukatili, kutokana na wahusika wa vitendo hivyo kuwa ni ndugu zao wa karibu au waume zao, kwa kuhofia kuvunja mahusiano, na kusababisha wahusika kutochukuliwa hatua, na vitendo hivyo vya ukatili kuendelea kuwepo na hatimaye kuleta madhara baadae ikiwamo kupoteza uhai, au mtoto kuambulia ujauzito.

 

Aidha amewaonya wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwalaza watoto chumba kimoja na wageni, bali wakalale nao, na chumba hicho wamuachie mgeni, kwa sababu wageni wengine ndio wamekuwa wahusika wakuu wa kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili kwa kuwachezea michezo michafu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso