WAZIRI MKUU DR MWIGULU NCHEMBA ATOA MAAGIZO UJENZI WA JENGO LA DHARURA HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA KUANZA MWAKA UJAO - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 11 November 2026

WAZIRI MKUU DR MWIGULU NCHEMBA ATOA MAAGIZO UJENZI WA JENGO LA DHARURA HOSPITALI YA MANISPAA YA KAHAMA KUANZA MWAKA UJAO

 




Na Neema Nkumbi, Kahama

WAZIRI MKUU, Dk. Mwigulu Nchemba, amemwelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama kukamilisha taratib

Du zote za kitaalamu na manunuzi kabla ya kumalizika kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ili ujenzi wa jengo la huduma za dharura (Emergency) katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, uanze mwanzoni mwa mwaka wa fedha unaofuata.

Dk. Nchemba ametoa maelekezo hayo leo Jumanne, Novemba 10, 2026, wakati akijibu hoja ya Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, aliyeiomba Serikali kuwezesha ujenzi wa jengo maalumu la huduma za dharura katika hospitali hiyo ili kukabiliana na changamoto za utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.

Waziri Mkuu amesema maandalizi ya mradi huo yanapaswa kukamilishwa mapema ili kuwezesha ujenzi kuanza kwa wakati, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Kahama na maeneo jirani.

“Nimepokea hoja kuhusu jengo la huduma za dharura Hospitali ya Kahama. Nakuelekeza Mkurugenzi, kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha, taratibu zote za kitaalamu pamoja na taratibu za manunuzi zikamilishwe ili tunapoanza mwaka ujao tuwe tayari kuanza ujenzi wa jengo hilo, wananchi wa Kahama na maeneo jirani wanufaike na huduma bora za dharura,” amesema Dk. Nchemba.

Awali, akitoa salamu za Jimbo la Kahama Mjini, Mbunge Benjamin Ngayiwa aliiomba Serikali kupandisha hadhi Hospitali ya Manispaa ya Kahama na kuifanya kuwa hospitali ya mkoa, sambamba na kujenga jengo la kisasa la huduma za dharura.

Ngayiwa amesema Kahama ina mwingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli za kiuchumi na usafiri wa kimataifa, hususan magari yanayosafiri kwenda Burundi, Rwanda, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hali inayoongeza mahitaji ya huduma za afya katika eneo hilo.

“Tunakuomba sana tupate jengo la wagonjwa wa dharura kwa ubora. Ukizingatia Kahama kuna mwingiliano mkubwa wa watu, magari yanayoenda Burundi, Rwanda, Uganda, Congo yote yanapita hapa,” amesema Ngayiwa.

Ameongeza kuwa licha ya hospitali hiyo kuwa na majengo na wataalamu wa afya, bado inakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na jengo la kisasa na maalumu la huduma za dharura, hali inayosababisha baadhi ya wagonjwa kuhitaji kupelekwa Mwanza kwa ajili ya kupata huduma zinazohitajika.

Utekelezaji wa maelekezo hayo unatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuboresha uwezo wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama kutoa huduma za dharura na kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa wanaohitaji matibabu ya haraka.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso