
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, amesema mamlaka hiyo imefanikisha kudhibiti mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya baada ya kukamata jumla ya paketi 753 za dawa hizo nchini Tanzania na Kenya, huku watuhumiwa saba wakikamatwa.
Akizungumzia na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam amesema operesheni hiyo ilianza Novemba 6, 2026, eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam, ambapo DCEA ilikamata paketi 299 za dawa za kulevya, zikiwemo paketi 24 za heroin na paketi 275 za methamphetamine.
Amesema dawa hizo zilikamatwa zikiwa zimefichwa ndani ya magari mawili aina ya Ford Ranger yenye namba za usajili T.950 ERA na T.417 EJZ, ambayo pia yanashikiliwa kutokana na kuhusishwa na uhalifu huo.
Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wanne walikamatwa ambao ni Juma Slaati Kisomeko (36), raia wa Uganda, dereva na mkazi wa Piji nchini Uganda; Issa Said Nassoro (34), mfanyabiashara; Ibrahim Said Chembela (30), dereva; na Mohamed Ally Shemtuu (45), dereva, ambao watatu wa mwisho ni wakazi wa Tabata, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Lyimo, baada ya kukamatwa na kuhojiwa, watuhumiwa hao walieleza kuwa dawa hizo walizichukua Mombasa, Kenya, na kuzisafirisha kuingia Tanzania kupitia mpaka wa Horohoro mkoani Tanga.
Kutokana na maelezo hayo, DCEA ilishirikisha mamlaka husika nchini Kenya, ambapo ushirikiano huo uliwezesha kubaini chanzo, eneo lililotumika kuhifadhi dawa hizo pamoja na kuwabaini wahusika wengine wa mtandao huo.
Amesema Novemba 7, 2026, DCEA kwa kushirikiana na Kitengo cha Kimataifa cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini Kenya (NANB), walifanikiwa kukamata paketi nyingine 454 za methamphetamine katika operesheni iliyofanyika eneo la Kwale, jijini Mombasa, Kenya.
Katika operesheni hiyo, watuhumiwa wengine watatu walikamatwa ambao ni Saleh Khamis Baseleman (45), maarufu kwa jina la Mbwiga, raia wa Tanzania, mfanyabiashara na mkazi wa Mombasa nchini Kenya; Seif Said Hamad (54), maarufu kwa jina la Babu Seif, maarufu kwa jina la Babu Seif, raia wa Tanzania, mvuvi na mkazi wa Kinondo, Mombasa; pamoja na Zuraicah Ahmed Hussein (25), raia wa Uganda, mfanyabiashara na mkazi wa Shirazi, Mombasa, nchini Kenya.
Lyimo amesema taratibu za kisheria kati ya Tanzania na Kenya zinaendelea ili kuhakikisha watuhumiwa wote wanafikishwa mbele ya vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.
Amesema baadhi ya watuhumiwa waliokamatwa ni vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya unaofanya shughuli zake katika nchi mbalimbali, zikiwemo Afghanistan, Afrika Kusini, Msumbiji, Zambia, Malawi, Uganda, Kenya, Tanzania na Dubai.
No comments:
Post a Comment