ABIRIA 52 WANUSURIKA KIFO, MILANGO YA BASI LA ABOOD YAZUA HOFU KWA MANUSURA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 13 November 2026

ABIRIA 52 WANUSURIKA KIFO, MILANGO YA BASI LA ABOOD YAZUA HOFU KWA MANUSURA

 


Manusura wasema walilazimika kujinusuru kupitia madirishani baada ya moto kuanza upande wa dereva na mlango wa nyuma kushindwa kufunguka.

Abiria 49 na wahudumu watatu wa basi la Kampuni ya Usafirishaji ya Abood wamenusurika kifo baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba, mkoani Kagera, kuteketea kwa moto katika eneo la Isaka, Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Tukio hilo limetokea leo Ijumaa, Novemba 13, 2026, majira ya saa 11 alfajiri, wakati basi hilo lenye namba za usajili T 285 EAV likiwa safarini, huku manusura wakieleza kuwa walikabiliwa na wakati mgumu kujiokoa baada ya moto kuanza kusambaa na mlango wa nyuma kushindwa kufunguka.

Kwa mujibu wa baadhi ya manusura, moto ulianza upande wa dereva, hali iliyosababisha taharuki ndani ya basi na kuwalazimu abiria kutafuta njia mbadala za kujiokoa, zikiwemo madirisha.

Ndabakiza Ndamuru, mfanyabiashara wa nguo kutoka nchini Burundi, amesema alikuwa akisafiri kutoka Dar es Salaam alikokwenda kuchukua mizigo ya biashara, lakini mali zake zimeteketea katika tukio hilo.

Akielezea namna walivyookoka, amesema moto ulipoanza upande wa dereva, abiria walilazimika kutoka kupitia madirishani ili kuokoa maisha yao.

“Ilikuwa saa 11 alfajiri, moto ulianzia huko mbele upande wa dereva, na hapo sisi tukaanza kutokea madirishani, Tunashukuru hakuna aliyeumia, Nilikuwa nimetoka Dar es Salaam kuchukua mzigo, umeteketea,” amesema Ndamuru.

Naye Beatrice Baitwa, mfanyabiashara wa nguo na viatu kutoka Bukoba, amesema hali ilikuwa ya kutisha baada ya abiria kushindwa kutumia mlango wa nyuma, huku moto ukiendelea kusambaa.

Amesema walipokuwa wamefika eneo la hospitali, mmoja wa abiria alianza kupiga kelele kuwa moto unawaka, lakini walipojaribu kutoka walibaini mlango wa nyuma ulikuwa umejifunga na haukufunguka.

“Wakati tunashtuka, huu mlango wa nyuma ukawa umejifunga, haufunguki, mlango mmoja tu wa mbele ndio ulikuwa wazi,” amesema Baitwa.

Ameongeza kuwa moto ulipozidi kuwa mkubwa, abiria walianza kusukumana katika harakati za kujiokoa, baadhi wakianguka huku wengine wakifanikiwa kutoka kupitia madirishani.

Baada ya kutoka nje, abiria hao walishirikiana kuokoa mizigo iliyokuwa kwenye sehemu za kuhifadhia mizigo za basi hilo. Hata hivyo, milango ya buti ilishindwa kufunguka, na walifanikiwa kufungua buti moja pekee na kuokoa baadhi ya mali, huku nyingine zikiendelea kuteketea.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Kahama,  Stanley Luhwago, amesema kikosi chake kilifika eneo la tukio na kufanikiwa kuuzima moto huo, ingawa sehemu kubwa ya mali zilizokuwa ndani ya basi ilikwishateketea.

Luhwago amesema basi hilo lilikuwa na abiria 49 na wahudumu watatu, wakiwemo madereva wawili, na kuthibitisha kuwa hakuna aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa.

“Tulianza kupambana na moto huo kuokoa mali zilizokuwemo, lakini basi hilo lilikuwa limeshaenea moto lote, na baadhi ya mali zimeshaungua, lakini tumefanikiwa kuuzima, Basi lilikuwa na abiria 49 na wahudumu watatu wakiwemo madereva wawili,” amesema Luhwago.

Aidha, amewataka madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa magari yao, hususan mifumo ya umeme, pamoja na kuhakikisha wanakuwa na vifaa vya kuzimia moto ili kuwezesha kukabiliana na matukio ya moto katika hatua za awali.

Amesema abiria wote walionusurika wameendelea na safari zao.

Hadi sasa, chanzo cha moto huo hakijajulikana, huku tukio hilo likisababisha uharibifu mkubwa wa basi na kupotea kwa baadhi ya mali za wafanyabiashara waliokuwa wakisafiri nalo.


www.huheso.co.tz


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso