NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA
Wananchi wa Kijiji cha Mwabomba, Kata ya Idahina, Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama, wameiomba serikali kuharakisha juhudi za upatikanaji wa kituo cha polisi katika eneo hilo ili kuimarisha usalama wa wananchi na kulinda shughuli zao za kiuchumi.
Ombi hilo limetolewa wakati wa ziara ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, kijijini hapo, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya makamanda wa polisi kuzungumza na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kuimarisha ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi.
Akizungumza katika ziara hiyo, mwananchi Sospeter Bulendi amesema ujambazi umepungua katika eneo hilo, hali anayoihusisha na ushirikiano uliopo kati ya wananchi na Jeshi la Polisi.
Bulendi amesema Mwabomba ina shughuli nyingi za kiuchumi, zikiwemo uchimbaji mdogo wa madini, kilimo na biashara, hivyo kuwa na kituo cha polisi kutasaidia kulinda maisha ya wananchi na mali zao.
Diwani wa kata ya Idahina Mathias Makashi amesema wananchi wanahitaji mazingira salama yatakayowawezesha kuendelea na shughuli zao za kiuchumi bila hofu ya uhalifu, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha huduma za kipolisi katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Kamanda Magomi amesema Jeshi la Polisi ni rafiki wa wananchi na kuwataka wasisite kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu na changamoto za usalama zinazowakabili.
Amesema serikali inataka wananchi, wakiwemo wachimbaji wadogo wa madini, wafanye shughuli zao katika mazingira salama yatakayowawezesha kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Akizungumzia usalama migodini, Magomi amewataka wachimbaji na wamiliki wa migodi kuzingatia taratibu za usalama ili kuzuia ajali zinazoweza kusababisha majeraha na vifo.
Pia amekemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, ikiwemo ubakaji, ulawiti na vipigo, huku akiwataka wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kutoa taarifa za matukio hayo ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Kuhusu ombi la kituo cha polisi, Magomi amesema kuna umuhimu wa kuboresha upatikanaji wa huduma za kipolisi katika eneo hilo na kuomba kuonyeshwa eneo linalopendekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho ili kuona uwezekano wa hatua zinazofuata.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi, viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi ni muhimu katika kudumisha amani, kuzuia uhalifu na kuwezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo.
Ekari mbili zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi kata ya Idahina.


















No comments:
Post a Comment