Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Iyomongi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mboni Mhita akizungumza na wajasiriamali wakati wa kufunga maonyesho ya Sido yaliyofanyika Kitaifa katika Wilaya ya Kahama.
NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA.
WAJASIRIAMALI walioshiriki Maonesho ya Kitaifa ya SIDO yaliyofanyika Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, wameiomba Serikali na wadau wa sekta binafsi kuweka mikakati madhubuti ya kuwapatia mitaji, mikopo yenye masharti nafuu na masoko ya uhakika ili kuwawezesha kukuza biashara zao na kuongeza mchango wao katika uchumi wa taifa.
Wamesema pamoja na jitihada wanazofanya kuzalisha bidhaa mbalimbali, bado wanakabiliwa na changamoto zinazohusiana na upatikanaji wa mitaji, gharama za uzalishaji, elimu ya biashara, viwango na ubora wa bidhaa pamoja na kukosa masoko ya uhakika.
Wakizungumza kupitia risala iliyosomwa na mwakilishi wao, Kassim Athuman Chacharika, wakati wa hafla ya kufunga maonesho hayo, wajasiriamali hao wameomba Serikali na taasisi zinazohusika na maendeleo ya biashara kuweka utaratibu utakaorahisisha upatikanaji wa mikopo na mitaji kwa wajasiriamali wadogo.
Pia wameomba kuongezewa elimu na mafunzo kuhusu viwango na ubora wa bidhaa, ufungashaji, usafirishaji na mbinu bora za uzalishaji ili bidhaa zao ziweze kukidhi mahitaji ya soko na kushindana na bidhaa nyingine.
Katika risala hiyo, wajasiriamali wameeleza kuwa changamoto nyingine ni upatikanaji wa masoko ya kutosha, huku wakiiomba Serikali kuongeza juhudi za kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini na kuwapa nafasi zaidi wajasiriamali kushiriki katika maonesho mbalimbali.
Aidha, wameomba kuangaliwa upya kwa baadhi ya gharama zinazohusiana na ushiriki wa maonesho ili kupunguza mzigo kwa wajasiriamali wadogo na kuwawezesha wengi zaidi kutumia fursa hizo kutangaza bidhaa zao na kutafuta wateja.
Wamezitaka pia taasisi za umma na wadau wa sekta binafsi kushirikiana katika kukuza biashara za ndani kwa kuhamasisha matumizi ya bidhaa zinazozalishwa nchini, hatua wanayoamini itachochea uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, David Iyomongi, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo, Mboni Mhita, amesema kuna umuhimu wa kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula nchini ili kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.
Iyomongi amesema Serikali hutumia takribani Sh bilioni 70 kwa mwaka kuagiza mafuta ya kula kutoka nje, hivyo amewataka wakulima, wajasiriamali na wachakataji kutumia fursa zilizopo katika kilimo na uchakataji wa mazao yanayozalisha mafuta.
Amesisitiza umuhimu wa kutumia mashine na teknolojia za kisasa katika uzalishaji na uchakataji wa bidhaa, akieleza kuwa upatikanaji wa nishati ya umeme ni miongoni mwa fursa zinazopaswa kutumiwa na wajasiriamali kuongeza uzalishaji.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza thamani ya mazao, kukuza viwanda vidogo na vya kati pamoja na kupunguza gharama zinazotumika kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa SIDO, Gervas Ntahumba, katika hotuba yake alieleza kuhusu utekelezaji wa maelekezo na mipango ya Serikali katika kuendeleza sekta ya viwanda na ujasiriamali, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza juhudi za kukuza shughuli za kiuchumi na kuwasaidia wajasiriamali.
Maonesho ya Kitaifa ya SIDO ni sehemu ya juhudi za kuwaunganisha wajasiriamali na wadau mbalimbali wa maendeleo ya biashara, kuwapatia fursa za kutangaza bidhaa zao, kujifunza teknolojia mpya na kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

















No comments:
Post a Comment