*KUENZI HAKI YA KUABUDU*
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam – 18 Oktoba, 2026
Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na madhehebu ya dini nchini, ikitambua mchango wake katika malezi ya kiroho, utoaji wa huduma za kijamii na kuimarisha amani na mshikamano wa kitaifa. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu, aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ibada takatifu ya kumweka wakfu Askofu John Jumanne Wambura wa Kanisa la Mennonite Tanzania (KMT), iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 18, 2026.
Akizungumza katika ibada hiyo, Mhe. Sangu amesema viongozi wa dini wameendelea kuwa nguzo muhimu katika kutoa mafundisho, ushauri na malezi bora, pamoja na kuwahudumia wananchi wenye mahitaji maalumu, wakiwemo yatima, wajane na watu wenye ulemavu.
Amesema Serikali inatambua mchango wa taasisi za dini katika sekta za afya, elimu na huduma nyingine za kijamii, hususan katika maeneo ya pembezoni, na kwamba ushirikiano huo ni muhimu katika kuharakisha maendeleo ya wananchi. Aidha, amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa na kuhamasisha jamii kulinda amani iliyopo nchini, akisisitiza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu iko tayari kushirikiana na wadau wote katika kuimarisha mshikamano na maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Mennonite Tanzania, Nelson Kisare, amewataka viongozi kutumia nafasi walizopewa kwa manufaa ya watu wanaowaongoza na jamii kwa ujumla, badala ya kujinufaisha binafsi. Amesema viongozi wanapaswa kuwa vielelezo vya maadili mema na matendo yanayojenga jamii. Huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amelishukuru Kanisa la Mennonite kwa kuendelea kuliombea Taifa na kuchangia juhudi za kudumisha amani nchini.

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
No comments:
Post a Comment