MISS SHINYANGA 2026 KUIBUA BALOZI WA UTAMADUNI NA FURSA ZA SHINYANGA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 4 October 2026

MISS SHINYANGA 2026 KUIBUA BALOZI WA UTAMADUNI NA FURSA ZA SHINYANGA



Mkurugenzi wa Holysmile ambaye pia ni Mratibu wa Miss Shinyanga 2026, Arnold Bweichum aliyevaa fulana nyeusi, akizungumza na waandishi wa habari  kuhusu mashindano ya walimbwende (miss Shinyanga) yanayofanyika  Oktoba 11, 2026 katika Wilaya ya Kahama.



NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA

Mkoa wa Shinyanga unatarajia kupata balozi mpya wa kutangaza utamaduni, vivutio na fursa mbalimbali za kiuchumi kupitia mashindano ya Miss Shinyanga 2026, yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 11, 2026 katika Wilaya ya Kahama.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuwakutanisha warembo kutoka maeneo mbalimbali ya mkoani Shinyanga, huku jumla ya washiriki 15 wakitarajiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kumpata mshindi atakayeuwakilisha mkoa huo katika mashindano ya Miss Kanda ya Ziwa, kabla ya kuelekea katika jukwaa la Miss Tanzania.

Mashindano hayo yanaandaliwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Holysmile Arnold Bweichum yenye makao makuu yake Kahama, ambayo imeanza maandalizi huku akiendelea kuomba ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara na taasisi, ili kufanikisha tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mashindano hayo, Mkurugenzi wa Holysmile ambaye pia ni Mratibu wa Miss Shinyanga 2026, Arnold Bweichum, amesema mshindi hatakuwa mwakilishi wa urembo pekee, bali atakuwa na jukumu la kuitangaza Shinyanga katika maeneo ya utamaduni, uchumi na uwekezaji.

Bweichum amesema hadi sasa wamepokea maombi ya warembo 21 waliojaza fomu za kushiriki, lakini ni washiriki 15 pekee watakaopata nafasi ya kuingia kwenye mashindano hayo.

Amesema mchakato wa kuchagua washiriki utafanyika kuanzia Oktoba 4 hadi 7, 2026, huku kilele cha mashindano hayo kikitarajiwa kuwa Oktoba 11, ambapo Miss Shinyanga 2026 atapatikana.


“Mpaka sasa tunayo maombi ya washiriki 21 waliojaza fomu, lakini watakaohitajika kushiriki ni 15 pekee. Mchakato wa kupata washiriki unaanza Oktoba 4 hadi 7 na Oktoba 11 ndiyo itakuwa kilele cha kumpata Miss Shinyanga 2026,” amesema Bweichum.

Aidha, amewataka majaji watakaosimamia mashindano hayo kuzingatia kikamilifu vigezo na kanuni zilizowekwa, akieleza kuwa haki na kutokuwa na upendeleo ni muhimu katika kulinda uaminifu na taswira ya mashindano.

Kwa upande wake, Ofisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mwaita Mwinyimkuu, amesema Manispaa hiyo itashirikiana na waandaaji kuhakikisha mchakato wa kumpata mshindi unafanyika kwa kuzingatia haki na usawa.

Mwinyimkuu amesema mshindi atakuwa na nafasi ya kutumia jukwaa hilo kuitangaza Shinyanga, hususan fursa za kiuchumi zinazopatikana katika mkoa huo, kwa lengo la kuwavutia wawekezaji katika sekta mbalimbali.

Naye Mwalimu wa Mitindo na Urembo, Cathbert Kowero, amesema maandalizi ya mashindano yatazingatia vigezo vya urembo na uwezo wa washiriki kuanzia kipindi cha kambi hadi siku ya fainali.

Akizungumza kuhusu matarajio yake, mmoja wa washiriki wa Miss Shinyanga 2026, Editha Shusho, amesema mashindano hayo yatawapa warembo nafasi ya kujenga mahusiano, kubadilishana uzoefu na kufahamu zaidi fursa zilizopo ndani ya Mkoa wa Shinyanga.

Shusho amesema akipata nafasi hiyo, atatumia jukwaa la Miss Shinyanga kuonyesha uwezo wake huku akiendelea kuhamasisha jamii kuhusu fursa za kiuchumi na kiutamaduni zinazopatikana mkoani Shinyanga.

Mmoja wa washiriki wa Miss Shinyanga 2026, Editha Shusho, akielezea matarajio yake endapo atachaguliwa kuwa miss Shinyanga.


Baadhi ya washiriki wa mashindano ya ulimbwende mkoani Shinyanga





No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso