ILELEMA GOLD MINE FC YAANDIKA HISTORIA MAHONA CUP, KDFA YATAKA TIMU ZISAJILIWE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 19 October 2026

ILELEMA GOLD MINE FC YAANDIKA HISTORIA MAHONA CUP, KDFA YATAKA TIMU ZISAJILIWE

 

Mkurugenzi wa Mahona Cup, Patrick Mahona akizungumza katika sherehe ya kujipongeza kwa timu ya Ilelema goldmine fc kutwaa ubingwa wa Mahona Cup, msimu wa 2025/2026, mzunguko wa 12.


NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA


Timu ya Ilelema Gold Mine FC imeibuka bingwa wa mashindano ya soka ya Mahona Cup msimu wa 2025/2026, huku viongozi wa soka wilayani Kahama wakizitaka timu za Halmashauri ya Msalala kusajiliwa rasmi ili ziweze kushiriki ligi na mashindano mbalimbali yanayotambuliwa na mamlaka za michezo nchini.

Akizungumza katika sherehe ya kujipongeza kutwaa ubingwa wa Mahona Cup, msimu wa 2025/2026, mzunguko wa 12, mmoja wa viongozi wa Ilelema Gold Mine FC, Henry Ntoba, amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu kwa timu hiyo, ambayo imeweza kutwaa ubingwa katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake.

Amesema uongozi wa timu hiyo una dhamira ya kuendeleza michezo na kuboresha miundombinu, ikiwamo kujenga uwanja wa kisasa utakaotumika kama uwanja wa nyumbani wa Ilelema Gold Mine FC na kuwawezesha wakazi wa Segese, Kahama na maeneo jirani kunufaika na shughuli mbalimbali za michezo.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Chama cha Mpira wa Miguu Kahama (KDFA), Paschal Malulu, amepongeza Ilelema Gold Mine FC kwa kutwaa ubingwa wa Maona Cup, huku akizitaka timu ambazo bado hazijasajiliwa kukamilisha taratibu za usajili ili zitambulike rasmi na kupata fursa za kushiriki mashindano mbalimbali.

Malulu amesema usajili rasmi utaziwezesha timu kutambulika na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na kupata sifa za kushiriki ligi za wilaya, mkoa na mashindano mengine yanayosimamiwa na mamlaka husika za soka, ikiwamo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa kuzingatia masharti ya kila mashindano.

Ameeleza kuwa KDFA inaendelea na majadiliano kuhusu uwezekano wa kuwa na ligi za wilaya katika Halmashauri ya Msalala na Halmashauri ya Ushetu, sambamba na Manispaa ya Kahama, ili timu nyingi zaidi zipate nafasi ya kushiriki mashindano katika maeneo yao.

Amesema changamoto mojawapo inayokabili maendeleo ya soka katika eneo hilo ni uhaba wa viwanja vyenye sifa za kuandaa ligi, hali inayosababisha michezo mingi kuchezwa katika Uwanja wa Taifa wa Kahama.

Kwa mujibu wa Malulu, ujenzi wa viwanja vya nyumbani na kuboresha miundombinu ya michezo kutasaidia kupanua wigo wa mashindano, kupunguza utegemezi wa uwanja mmoja na kutoa fursa kwa chama cha soka kupeleka ligi karibu zaidi na wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Mahona Cup msimu wa 2021/2022, Hussein Issa, amesema mashindano hayo yameendelea kukua na kuboresha ushindani wake, akieleza kuwa mafanikio ya msimu huo ni hatua ya kujivunia kwa waandaaji na wadau wa michezo.

Issa amemshukuru Diwani wa Kata ya Segese, Patrick Mahona, kwa kuwaamini waandaaji na kuwapa nafasi ya kusimamia mashindano hayo, akisema ushirikiano huo umechangia kufanikisha mashindano yaliyowakutanisha wakazi wa Segese na maeneo mbalimbali ya Kahama.

Kwa upande wake, Nahodha wa Ilelema Gold Mine FC, Cheche Damas, amemshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na uongozi wa timu na wakazi wa kijiji cha Ilelema kwa mchango wao ulioiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa.

Damas amesema timu ilifanya maandalizi na kupata wachezaji wenye uwezo, jambo lililochangia mafanikio hayo, huku akieleza kuwa mashindano hayo yamewapa wachezaji fursa ya kuonyesha vipaji vyao na kuongeza mwamko wa michezo kwa wakazi wa eneo hilo.

Ameongeza kuwa mashindano kama Mahona Cup yana umuhimu mkubwa kwa jamii kwa kuwa yanatoa burudani, yanaunganisha wananchi na kuwashirikisha vijana katika shughuli za michezo, hatua inayoweza kuwasaidia kutumia muda wao katika shughuli zenye manufaa.

Damas amewataka waandaaji kuendelea kuandaa mashindano hayo katika misimu ijayo, akisema mafanikio yake yanaonyesha umuhimu wa kuwekeza katika michezo na kuendeleza vipaji vya vijana.

Mkurugenzi wa Mahona Cup, Patrick Mahona amesema anapoandaa mashindano na kombe linatoka nje ya mji na kuchukuliwa na watu wa pembezoni mwa mji linampa hamasa ya kuandaa mashindano zaidi.

" Mimi kama mwandaaji wa mashindano ninapoandaa mashindano na kombe likachukuliwa na washindi kutoka nje ya mji inanipa hamasa ya kuandaa mashindano zaidi maana kama kombe linabaki palepale kila siku nakuwa sinahaja ya kuandaa mashindano" amesema Mahona.


Mahona amewashukuru wote wanaomuunga mkono, uongozi wa chama cha mpira wa miguu Wilaya ya Kahama, Mkoa hata taifa, pia ameuomba uongozi wa wilaya kutuma wataalamu wa kutengeneza viwanja vya michezo kuunga mkono juhudi za mkurugenzi wa Ilelema goldmine fc ambaye amenunua eneo kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha mpira wa miguu.

Amesema uwanja ukijengwa watapata maendeleo katika kijiji hicho kwani wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza na biashara mbalimbali na kuongeza pato la halmashauri.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso