Tanzania imeendelea kujitengenezea taswira nzuri kimataifa na kuvutia umati wa wageni, wawekezaji, na wanunuzi kutoka pande zote za dunia kufuatia ushiriki wake madhubuti katika Maonesho ya Kimataifa ya Vito na Saa ya Doha (Doha Jewellery & Watches Exhibition – DJWE) 2026, yanayofanyika jijini Doha, Qatar.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, umemtumia fursa hiyo ya kipekee kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 3, 2026, kuitangaza nchi, rasilimali zake za asili, na hususan madini ya kipekee ya Tanzanite, huku ukiwavutia wageni na wadau wa kimataifa kuja kuwekeza katika sekta ya madini nchini.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Kiruswa alisisitiza kuwa maonesho hayo yamekuwa nguzo muhimu ya kujenga mahusiano ya kibiashara na kutangaza fursa tele za uwekezaji zilizopo nchini katika nyanja za utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, na uongezaji thamani wa madini ya vito.
Alifafanua kuwa ushiriki huo unalenga kuwaonesha wageni na wawekezaji wa kimataifa utajiri mkubwa wa rasilimali za Tanzania, huku serikali ikiweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha bidhaa za madini zinaongezewa thamani nchini kabla ya kusafirishwa kwenda masoko ya nje.
Maonesho hayo ya DJWE 2026 yamewakutanisha wazalishaji, wafanyabiashara, na wataalamu wakubwa wa sekta ya vito kutoka kote duniani, hali iliyowapa wafanyabiashara wa Kitanzania waliouambatana na ujumbe huo fursa adhimu ya kujionea mwenendo wa soko la kimataifa, kujenga mitandao ya kibiashara, na kuvutia wageni kutembelea na kufanya biashara na wazawa.
Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Mohamed, naye aliahidi kuendelea kusimama mstari wa mbele katika kutangaza fursa hizo ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi na kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini ya Vito Tanzania (TAMIDA), Osman Abdulsattar, ameipongeza Serikali kwa kuwawezesha kushiriki, akieleza kuwa hatua hiyo imewakutanisha moja kwa moja na wanunuzi wakubwa wa kimataifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Kitanzania.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Al Fardan Investment Cooperation na mwandaaji wa maonesho hayo, Hussein Al Fardan, ameipongeza Tanzania kwa kuonyesha nia thabiti ya kushiriki, akibainisha kuwa iwapo Tanzania itashiriki rasmi kama nchi katika maonesho hayo mwaka ujao, itakuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufanya hivyo kwenye jukwaa hilo kubwa la kimataifa, huku akiahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa washiriki na wageni kutoka Tanzania.


No comments:
Post a Comment