SAMAMBA: TUTAFUNGA MIGODI ITAKAYOKIUKA USALAMA WA WACHIMBAJI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 28 September 2026

SAMAMBA: TUTAFUNGA MIGODI ITAKAYOKIUKA USALAMA WA WACHIMBAJI

 

Katibu Mtendaji wa Wizara ya Madini, Aziza Swedi, akizungumza na wachimbaji, wamiliki mameneja wa migodi na maafisa madini katika wilaya ya Kahama,

Na Neema Nkumbi, Kahama


Serikali imesema iko tayari kuchukua hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunga migodi, endapo itabainika kuwa wamiliki na waendeshaji wake wanakiuka kanuni za usalama na kuhatarisha maisha ya wachimbaji.


Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, wakati akizungumza na wachimbaji, wamiliki mameneja wa migodi na maafisa madini katika wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, katika mafunzo yanayolenga kuongeza uelewa kuhusu usalama wa migodi wakati wa kipindi cha mvua kubwa kinachotarajiwa.


Samamba amesema maisha ya mchimbaji yana thamani kubwa kwa familia, jamii na taifa, hivyo masuala ya uzalishaji hayapaswi kutangulizwa mbele ya usalama wa binadamu.


“Tutakuwa wakali na tutachukua hatua kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo, hasa kanuni zile za usimamizi wa mazingira na usalama migodini, Na ikiwezekana tutafunga migodi,” amesema.


Amesema hatua hiyo siyo chaguo linalopendelewa kwa sababu shughuli za madini zina mchango katika uchumi na ajira, lakini serikali haiwezi kuruhusu shughuli za uchimbaji kuendelea endapo maisha ya wachimbaji yanawekwa hatarini.


Akizungumzia kipindi cha mvua kubwa kinachotarajiwa, Samamba amesema migodi inapaswa kuweka taratibu maalum za kukabiliana na hali hiyo, ikiwemo kusimamisha shughuli za chini ya ardhi wakati mvua kubwa ikiendelea na kuruhusu wachimbaji kuingia baada ya eneo kukaguliwa na kuthibitishwa kuwa salama.


Ametaja miongoni mwa hatari zinazoweza kuongezeka wakati wa mvua ni kuporomoka kwa udongo na kuta za migodi, mafuriko kuingia chini ya ardhi, kudhoofika kwa nguzo za kuimarisha migodi na kujaa kwa maji katika maeneo ya uchimbaji.


Samamba pia amewataka wachimbaji kutotumia nguzo zilizoachwa chini kwa ajili ya usalama kama chanzo cha kuongeza uzalishaji, akisema hatua hiyo inaweza kuhatarisha uimara wa mgodi na maisha ya wachimbaji wanaoendelea na shughuli katika maeneo hayo.


Katika hatua nyingine, amesisitiza umuhimu wa kila mgodi kuwa na winchi mbili, ambapo moja itatumika katika shughuli za kawaida na nyingine iwe tayari kwa dharura ili kusaidia kuwaokoa wachimbaji endapo winchi ya kwanza itapata hitilafu.


Pia amesisitiza kuwa wakati wa mvua kubwa, mchimbaji hapaswi kuingia chini ya ardhi akiwa peke yake, bali angalau watu wawili wawe pamoja kwa ajili ya kusaidiana endapo dharura itatokea.


Kuhusu ulipuaji, Samamba amesema wachimbaji wanapaswa kutoka nje ya eneo la mgodi kwa umbali wa angalau mita 100 kabla ya ulipuaji, huku mtu akiruhusiwa kushuka tena chini baada ya kusubiri angalau dakika 30, ili kutoa muda kwa hewa chafu na gesi zinazoweza kuzalishwa na milipuko kuondoka.


Ametaka pia migodi kujenga na kusafisha mitaro inayozunguka midomo ya migodi, kuweka kinga dhidi ya maji ya juu, kuimarisha kuta na sehemu za hatarishi kwa kutumia mawe, zege au chuma kulingana na mahitaji ya usalama.


Aidha, ametoa maagizo ya kuongezwa kwa ukaguzi wa mabwawa ya mabaki ya migodi (TSF), akitaka kuhakikisha mabwawa hayo yana uwezo na uimara wa kutosha kupokea ongezeko la maji wakati wa mvua kubwa, huku kingo zake na maeneo mengine muhimu yakikaguliwa mara kwa mara.


Samamba amesisitiza pia kila mgodi kuwa na pampu ya maji inayofanya kazi na kuwa na mafuta ya kutosha wakati wote, badala ya kusubiri maji yaingie ndipo kuanza kutafuta vifaa vya kuyatoa.


Amesema mazingira ya migodi yanapaswa pia kuzingatia usafi, ikiwemo uwepo wa vyoo na usimamizi mzuri wa maji, ili kuzuia kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu wakati wa mvua kubwa.


Kwa upande wa utayari wa kukabiliana na majanga, Samamba amewataka mameneja na wamiliki wa migodi kuhakikisha kila mgodi una mpango wa dharura unaoeleweka kwa wafanyakazi, unaoainisha nani atatoa taarifa, taarifa itapelekwa wapi, shughuli zitasimamishwa wakati gani na namna ya kupata msaada wa serikali.


Pia amewataka maafisa madini kuhakikisha wachimbaji wanapata kwa wakati taarifa za utabiri wa hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili hatua za tahadhari zichukuliwe mapema.


Samamba amesema serikali itaendelea kusimamia maendeleo ya sekta ya madini, lakini usalama wa wachimbaji utabaki kuwa jambo la msingi, akieleza kuwa ajali inaweza kusababisha vifo, ulemavu wa kudumu, kupoteza nguvu kazi ya taifa na kuwaacha familia katika hali ya utegemezi.


Amewataka maafisa madini kufanya kazi kwa ushirikiano na wachimbaji badala ya kutumia maelekezo pekee, huku akiwataka washiriki wa mafunzo hayo kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia kutengeneza maazimio ya pamoja ya kuimarisha usalama wa migodi wakati wa kipindi cha mvua kubwa.


Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amewataka wachimbaji wa madini wilayani Kahama kuzingatia usalama katika shughuli zao, hususan katika msimu huu wa mvua unaotarajiwa kuwa na kiwango kikubwa cha mvua, akisema maji yanaweza kusababisha madhara katika maeneo yao.

Ngayiwa ameiomba Wizara ya Madini kuendelea na mpango wa kuwawezesha wachimbaji kupata vifaa vya uchimbaji, ikiwemo kompresor, winchi, vifaa vya kubondea na kuchoronga mawe pamoja na mashine za kusaga mawe, ili kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uzalishaji.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu tawala Wilaya ya Kahama, Tumshukuru Mdui amesema wilaya ya Kahama wamejiandaa vya kutisha kukabiliana na dharura zitakazojitokeza wakati wa mvua za el nino huku akiwataka wachimbaji kuchukua tahadhari mapema kulingana na hali ya hewa pia  kuendelea kufuatilia matangazo ya serikali ili kupata taarifa sahihi za hali ya hewa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso