PROF. MANYILIZU ACHANGIA VIFAA VYA MILIONI 2 SHULE YA NYASHIMBI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 22 September 2026

PROF. MANYILIZU ACHANGIA VIFAA VYA MILIONI 2 SHULE YA NYASHIMBI

 



KAHAMA, SHINYANGA

Prof. Majuto Clement Manyilizu, amechangia vifaa vya kisasa vya kielektroniki vyenye thamani ya Sh milioni mbili kwa Shule ya Msingi Nyashimbi iliyopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kutatua changamoto za vifaa vya kufundishia na kujifunzia shuleni hapo.

Vifaa hivyo ambavyo ni kompyuta na mashine ya kuchapa (printer), vinatarajiwa kusaidia kurahisisha uchapishaji wa mitihani na taarifa mbalimbali za shule hiyo.

Prof. Manyilizu alikabidhi vifaa hivyo wakati wa mahafali ya wahitimu wa darasa la saba mwaka 2026 yaliyofanyika Septemba 18 katika Ukumbi wa Gamma Hotel, Manispaa ya Kahama.

Akizungumza katika mahafali hayo, Prof. Manyilizu, ambaye pia ni mzaliwa wa Mtaa wa Nyashimbi, aliwaasa wahitimu kuwa makini katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana na jamii kwa ujumla, akisisitiza umuhimu wa kulinda maadili, kuzingatia elimu na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.

Alisema elimu ya msingi ni hatua muhimu katika maisha ya mtoto kwa kuwa ndiyo inayomjengea uwezo wa kusoma, kuandika na kuhesabu, sambamba na kuweka msingi wa maadili na kumwandaa kukabiliana na changamoto za maisha.

Prof. Manyilizu alitumia kifupi cha neno “MTAUMA” kueleza changamoto sita zinazowakabili vijana na jamii, ambazo ni Maadili, Teknolojia, Ajira, Uraibu, Mwili na Akili.

Akizungumzia suala la maadili, alisema mmomonyoko wa maadili ni changamoto inayojitokeza katika makundi mbalimbali ya jamii, hivyo aliwahimiza wahitimu kuzingatia mafundisho mazuri ya dini, kumheshimu Mungu, wazazi na watu wengine, pamoja na kuheshimu miili yao.

Kuhusu matumizi ya teknolojia, Prof. Manyilizu alisisitiza kuwa teknolojia ina mchango mkubwa katika maendeleo, lakini matumizi yasiyodhibitiwa, hasa ya mitandao ya kijamii na baadhi ya maudhui ya televisheni, yanaweza kuwa na athari kwa watoto na vijana.

Aliwataka wazazi kuwa makini katika kuwaongoza watoto wao wanapotumia teknolojia ili kuwakinga dhidi ya maudhui yanayoweza kuathiri maadili na afya yao ya akili.

Akizungumzia changamoto ya ajira, alisema ni suala linaloikabili dunia kwa ujumla, hivyo aliwahimiza wahitimu kuendelea kusoma na kuwekeza katika elimu ili kujiandaa na fursa za baadaye.

Alibainisha kuwa maeneo ya sayansi, teknolojia na uhandisi ni miongoni mwa sekta zinazohitaji wataalamu, huku akiwataka vijana kutokata tamaa wala kukatisha masomo kwa kukimbilia ajira zisizo rasmi, ndoa au kujiingiza katika uhalifu.

Katika eneo la uraibu, aliwataka vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, unywaji wa pombe kupita kiasi, kamari, kubashiri na matumizi yasiyofaa ya vinywaji vya kuongeza nguvu, akieleza kuwa tabia hizo zinaweza kuathiri afya ya mwili na akili.

Aidha, aliwasisitiza wahitimu kuzingatia afya ya mwili kwa kufanya mazoezi, kula vyakula vinavyofaa na kuepuka mitindo ya maisha inayoweza kuongeza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.

Kuhusu afya ya akili, alisema vijana wanapaswa kushirikisha wazazi, walimu na watu wazima wanaowaamini wanapokabiliwa na changamoto, ili waweze kupata ushauri na msaada unaofaa.

Aliongeza kuwa kupata usingizi wa kutosha na kufanya mazoezi ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia katika kutunza afya ya akili.

Kwa upande wa changamoto za shule hiyo, zilizowasilishwa kupitia risala ya wahitimu, Prof. Manyilizu alisema utatuzi wake unahitaji ushirikiano wa uongozi wa shule, serikali, wazazi, wananchi na wadau wa maendeleo.

Changamoto hizo ni pamoja na utoro wa mara kwa mara, upungufu wa madarasa, madawati na walimu, ukosefu wa chakula cha mchana kwa wanafunzi pamoja na kutokuwepo kwa mashine ya kuchapa mitihani.

Alishauri uongozi wa shule kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Nyashimbi pamoja na wazazi kutafuta suluhisho la utoro na changamoto ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.

Pia alieleza kuwa atazifikisha changamoto za shule hiyo katika Mkutano Mkuu wa Kahama Development Initiative (KADI) unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu, ili kujadili namna ya kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuzitatua.

Prof. Manyilizu, ambaye ni Katibu Mkuu Msaidizi wa KADI, alisema jumuiya hiyo ina malengo ya kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Kahama, ikiwemo katika sekta za elimu na afya.

Alisema pia kuna mpango wa kuwashirikisha wanachama wa KADI kuwa walezi wa shule mbalimbali ili wawe karibu na uongozi wa shule na kusaidia kutafuta ufumbuzi wa changamoto zake.

Katika hatua nyingine, aliwakumbusha wahitimu, wazazi na wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua nyingi zinazoweza kujitokeza katika ukanda wa Afrika Mashariki, akieleza kuwa taarifa za kisayansi alizozitaja zinaashiria uwezekano wa mvua kuwa juu ya wastani kutokana na hali ya El Niño.

Alisema mvua nyingi zinaweza kusababisha mafuriko, kubomoka kwa nyumba, kuharibika kwa miundombinu ya barabara, umeme na maji, pamoja na kuibuka kwa magonjwa.

Aliwataka wananchi kujiandaa na kuchukua tahadhari zinazofaa ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.

Awali, Prof. Manyilizu aliwapongeza uongozi wa shule chini ya Mwalimu Mkuu Mandalu John Lutelemla, walimu, wazazi, wanafunzi, viongozi wa serikali za mitaa na wadau wengine kwa mchango wao katika kuboresha elimu na kufanikisha mahafali hayo.

Akihitimisha hotuba yake, aliwakumbusha wahitimu kutunza roho, miili, hisia na akili zao, akisema ni muhimu kwa mafanikio yao binafsi, familia, jamii, taifa na dunia kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso