WADAU WAPONGEZA POLISI KUFUNGUA MILANGO YA SIASA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 5 August 2026

WADAU WAPONGEZA POLISI KUFUNGUA MILANGO YA SIASA



Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kuanza kupokea rasmi maombi ya vyama vya siasa na wanasiasa wenye nia ya kufanya mikutano ya hadhara na shughuli nyingine za kisiasa kufuatia kuimarika kwa hali ya usalama nchini.


Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo, Kamishna Msaidizi wa Polisi David Misime, imeeleza kuwa hatua hiyo inakuja baada ya mafanikio ya oparesheni zilizofanywa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, ambazo ziliwezesha kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa 130 waliokuwa wakipanga au kuratibu vitendo vya kihalifu, ikiwemo maandamano yasiyo rasmi, njama za kuchoma moto shule na kulipua transfoma za TANESCO.




Uamuzi huu unafuatia kusitishwa kwa muda kwa mikutano yote ya hadhara ya kisiasa kulikotangazwa Juni 26, 2026 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alipokuwa akizungumza bungeni jijini Dodoma ili kulinda usalama wa wananchi dhidi ya viashiria vya vurugu. Kufuatia kuondolewa kwa zuio hilo, Misime amewataka wote wenye nia ya kufanya mikusanyiko hiyo kuwasilisha taarifa zao kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya husika kwa mujibu wa sheria ili kupata ulinzi stahiki.


Akizungumzia tamko hilo, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amesema kuwa yanasubiriwa mazungumzo rasmi na viongozi wa vyama vya siasa kupitia vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa, kauli iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Juma Ali Khatibu, aliyempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IJP) Camillus Wambura na kuwataka wanasiasa kutumia fursa hiyo kunadi sera huku wakitumia lugha za staha zinazolinda amani ya nchi.


Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga, amekumbusha kuwa kufanya mikutano ya kisiasa ni haki ya kikatiba na sio hisani, akiwataka viongozi wa vyama kufuata taratibu za kutoa taarifa polisi ili kuwezesha usalama wao wakati wote wa shughuli zao.


Kwa upande wao, wadau wa siasa akiwemo aliyekuwa mgombea urais kupitia ADC, Wilson Mulunde na mwenzake wa UMD, Mwajuma Mirambo, wamepongeza uamuzi huo huku wakiiomba serikali kuchukua hatua dhidi ya wahusika binafsi wa vurugu badala ya kuadhibu vyama vyote, huku wananchi wakisisitiza umuhimu wa mikutano hiyo kuendeshwa kwa amani na kulinda heshima ya taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso