Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Buduba kata ya Nyandekwa manispaa ya KahamaNA NEEMA NKUMBI, KAHAMA
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema tayari Serikali imetenga Sh milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha kituo kimoja cha afya katika maeneo ya Nyandekwa au Mondo, huku akianza harakati za kutafuta Sh milioni 200 ili vituo vyote viwili viweze kukamilishwa kwa wakati mmoja.
Ngayiwa ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Kata ya Nyandekwa, Manispaa ya Kahama, ambako amezungumza na wananchi na kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa huduma za afya, maji, umeme, elimu na miundombinu.
Akizungumza mbele ya wananchi wa Kijiji cha Buduba, Mbunge huyo amesema suala la kukamilisha vituo vya afya vya Nyandekwa na Mondo limekuwa moja ya mambo anayoyafuatilia kwa karibu, kutokana na umuhimu wa huduma hizo kwa wananchi.
Amesema awali aliomba taarifa kuhusu kiasi kinachohitajika kukamilisha kituo cha afya cha Nyandekwa na alielezwa kuwa takribani Sh milioni 200 zingetosha kukamilisha kituo hicho.
“Nimeomba takwimu pale inahitaji shilingi ngapi? Nikaambiwa milioni mia mbili itatosha kukamilisha kile kituo. Sasa nimeomba vituo viwili, kwa sababu kuna kituo hiki cha Nyandekwa na kuna kituo cha afya kiko Mondo,” amesema Ngayiwa.
Mbunge huyo amesema taarifa alizopokea zinaonyesha kuwa tayari Sh milioni 200 zimepatikana kwa ajili ya kituo kimoja, lakini bado haijawa wazi fedha hizo zimeelekezwa katika kituo cha Nyandekwa au Mondo.
Kutokana na hali hiyo, amesema hataki kuona kituo kimoja kikipewa kipaumbele huku kingine kikiachwa, badala yake anataka kutafuta fedha za kutosha ili vituo vyote viweze kukamilishwa.
“Sasa nimeomba vituo viwili... habari njema nilizoambiwa ni kwamba tumepata shilingi milioni mia mbili kwa kituo chetu kimoja. Taarifa zingine zinasema ni kituo cha Mondo, kingine kinasema ni kituo cha Nyandekwa sasa sijajua ni kituo gani hasa,” amesema.
Amesema kwa kuwa Nyandekwa iko mbali na huduma za mjini, wananchi wake wana uhitaji mkubwa wa kuwa na kituo cha afya kinachofanya kazi kikamilifu.
Ngayiwa amesema lengo lake sasa ni kuhakikisha anapata jumla ya Sh milioni 400, kiasi ambacho kitasaidia kukamilisha vituo hivyo viwili.
BUDUBA YAPATA MSAADA WA ELIMU
Katika ziara hiyo, Ngayiwa pia ameeleza namna ujenzi wa miundombinu ya elimu ulivyopewa kipaumbele Buduba.
Amesema wakati wa kampeni, yeye pamoja na viongozi wenzake waliona hali ya madarasa katika eneo hilo na kuahidi kuboresha mazingira ya kujifunzia.
“Tulikuja hapa tukaangalia lile jengo la madarasa yetu lilivyokuwa limedondoka na tukaahidi kwamba pale mtakapotuchagua... kitu cha kwanza tutakachokifanya kwa Buduba, ni kuhakikisha yale madarasa yanajengwa na wanafunzi wetu wanarudi kusoma sehemu safi, bora na salama,” amesema.
Mbunge huyo amesema ahadi hiyo imeanza kutekelezwa, huku akieleza kuwa tayari shilingi milion 9.5 zimetumika katika ujenzi wa madarasa na ofisi katika eneo hilo.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali katika Kata ya Nyandekwa, ikiwemo maji, umeme, barabara na mikopo kwa vikundi vya wananchi.
VIKUNDI VIWILI VYA BUDUBA VYAPATA MIKOPO
Ngayiwa amesema kati ya vikundi vitano vilivyopata mikopo katika Kata ya Nyandekwa, vikundi viwili vinatoka Buduba.
Amesema hatua hiyo inaonyesha namna Serikali inavyoendelea kutoa fursa kwa wananchi kupitia mikopo ya vikundi.
“Kati ya vikundi vitano katika kata hii, viwili vinatoka hapa Buduba unaweza ukaona jinsi ambavyo Serikali yenu inajitahidi kuwafikia ninyi wananchi,” amesema.
DIWANI AORODHESHA MIRADI YA MAENDELEO
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Nyandekwa Rutahondi Katoto amempongeza Mbunge Ngayiwa kwa mchango wake katika kusukuma miradi ya maendeleo, akitaja ujenzi na ukarabati wa madarasa, umeme, barabara, ofisi ya kata, maji na mikopo kwa vikundi.
Diwani amesema Sh milioni 49.5 zilitolewa kwa ajili ya kukamilisha madarasa matatu na ofisi moja, huku Sh milioni 10 zikitumika kukarabati madarasa matano.
Katika sekta ya nishati, amesema vitongoji vitano vimepata fursa ya kuunganishwa na umeme kupitia mradi wa REA, huku vitongoji saba vikiwa vimefanyiwa surveying kwa ajili ya maandalizi ya kupelekewa huduma hiyo.
Aidha, amesema Sh milioni 54.2 zimetolewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Kata ya Nyandekwa, huku fedha nyingine zikitolewa kwa ajili ya barabara na ukarabati wa visima vitatu.
BUDUBA YATAKA HUDUMA ZA AFYA NA MAJI
Katika taarifa iliyowasilishwa kwa Mbunge na mtendaji wa kijiji Febrick Maige ameeleza kuwa kijiji hicho hakina zahanati, hivyo wananchi hulazimika kupata huduma za afya katika Kijiji cha Kakebe.
Kijiji hicho pia kinakabiliwa na changamoto ya maji katika Shule ya Msingi Buduba, huku wanafunzi na walimu wakilazimika kutafuta maji kwa majirani.
Uongozi umeomba takribani Sh milioni 1.925 kwa ajili ya kuunganisha maji katika shule hiyo.
Pamoja na changamoto hizo, Buduba inaendelea kunufaika na miradi ya maendeleo katika elimu, nishati na uwezeshaji wa wananchi, huku Mbunge Ngayiwa akiahidi kuendelea kushirikiana na viongozi wa kata na Serikali kuhakikisha changamoto zilizobaki zinapatiwa ufumbuzi.
Mwonekano wa madarasa mapya ya;iyojengwa kupitia mfuko wa jimbo yaliyogharimu shiling milioni 9.5
Mwonekano wa madarasa yaliyopo sasa ambayo wanafunzi wa shule ya msingi Buduba wanayatumia




No comments:
Post a Comment