Na Neema Nkumbi, Kahama
Waziri wa Nishati na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga, Deogratius Ndejembi, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kumsimamia mkandarasi ili aweze kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya Kahama–Kakola yenye urefu wa kilomita 73.1, akisisitiza kuwa Serikali imetenga fedha za mradi huo na wananchi wanapaswa kuanza kuona matokeo kwa wakati.
Ndejembi ametoa agizo hilo leo baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo inayounganisha maeneo ya Kahama Mjini na Msalala, akisema Serikali haina mashaka na ubora wa kazi inayofanywa na mkandarasi, bali kinachohitajika ni kuongeza kasi ya utekelezaji.
“Sina mashaka na kiwango chake, tumewaona lami hii ni lami nzuri. Sina mashaka na kiwango chake, lakini haongezi spidi ya ujenzi. Ongezeni spidi kuhakikisha kwamba inakamilika kwa wakati,” amesema Ndejembi.
Amesema fedha za mradi huo tayari zimetengwa na si suala la kusubiri fedha kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali, hivyo mkandarasi anapaswa kuongeza kasi ya kazi na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo kwa wakati.
“TANROADS, ongezeni spidi. Ongezeni spidi kazi hii ikamilike kwa wakati. Mradi huu na fedha zote zimeisha tengwa. Sio za kusubiri Mfuko Mkuu wa Serikali ndio alipwe. Tunachotaka kuona ni barabara inakamilika,” amesema.
NDEJEMBI AAGIZA TAA ZIFUNGWE MAPEMA
Mbali na kuongeza kasi ya ujenzi, Ndejembi ameitaka TANROADS kuanza kuweka taa za barabarani katika maeneo ambayo ujenzi wake umekamilika, badala ya kusubiri kilomita zote 73.1 zikamilike.
Amesema hatua hiyo itawezesha wananchi kuanza kunufaika na miundombinu hiyo mapema, huku ikiongeza usalama kwa watumiaji wa barabara wakati wa usiku.
“Msisubiri mpaka tumalize kilomita 73. Maeneo yanayokamilika, katika hizi kilomita 32 ambazo zimekamilika, anzaeni kufunga taa za barabarani, wananchi hawa waanze kuona taa zinawaka,” amesema.
Waziri huyo amesema maelekezo hayo yanaendana na msimamo wa Serikali wa kuhakikisha maeneo yenye barabara zinazokamilika yanawekewa taa kwa ajili ya kuongeza usalama na kurahisisha matumizi ya miundombinu hiyo.
MRADI WAFIKIA ASILIMIA 75.79
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 75.79, huku kiwango kilichotarajiwa katika kipindi hicho kikiwa takribani asilimia 88.3.
Hali hiyo inaonyesha kuwa mradi ulikuwa nyuma kwa takribani asilimia 12.5, hivyo Serikali inaendelea kusimamia kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha kazi inakamilika ndani ya muda wa mkataba.
Mwaikokesya amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kuunganisha Kahama na maeneo mengine pamoja na mikoa jirani, ikiwemo Geita na Mwanza.
Amesema mradi huo unapita katika maeneo mbalimbali yakiwemo Manzese, Tia, Karagwa, Segese hadi Kakola, huku ukitekelezwa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa wakati wa ukaguzi, muda wa mkataba wa mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba 4, 2026.
NGAYIWA: SAFARI YA SAA MBILI KUPUNGUA HADI DAKIKA 40–50
Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, amesema barabara hiyo imekuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi, lakini kukamilika kwake kutabadilisha kwa kiasi kikubwa usafiri na shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo.
Ngayiwa amesema awali safari kutoka Kahama hadi Kakola ilikuwa ikichukua takribani saa mbili, lakini baada ya kukamilika kwa barabara hiyo muda huo unaweza kupungua hadi dakika 40–50.
“Kutoka Kahama kwenda Kakola tulikuwa tunatumia takribani masaa mawili. Lakini kwa ujenzi na ukamilishaji wa barabara hii, sasa kwenda Kakola kutoka Kahama itachukua kama dakika hamsini mpaka arobaini,” amesema.
Amesema barabara hiyo ni muhimu kutokana na kuunganisha maeneo yenye shughuli za uchimbaji mdogo na mkubwa wa dhahabu, hivyo kuboreshwa kwa usafiri kutasaidia kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi.
Ngayiwa amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, akisema wananchi wameupokea kwa mikono miwili.
MANGILA: BARABARA ITACHOCHEA MADINI, KILIMO NA VIWANDA
Mbunge wa Msalala, Mabula Mangila, amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutafungua fursa kubwa za kiuchumi katika jimbo hilo, likiwemo eneo la madini, kilimo, viwanda na ajira.
Mangila amesema Jimbo la Msalala lina kata 18 zenye shughuli mbalimbali za uzalishaji, huku maeneo mengi yakiwa na fursa za uchimbaji wa madini pamoja na kilimo, ikiwemo kilimo cha mpunga.
Amesema barabara hiyo itapandisha thamani ya maeneo yaliyopo pembezoni mwa barabara na kuvutia wawekezaji kuanzisha viwanda.
“Barabara hii inakwenda kupandisha thamani ya maeneo yetu, viwanda vyetu vya wananchi ambao wako pembezoni mwa hii barabara. Lakini barabara hii inakwenda kuvutia uwekezaji zaidi wa viwanda katika ukanda wetu wa Halmashauri ya Msalala,” amesema Mangila.
Amesema uwepo wa miundombinu bora ni muhimu kwa wawekezaji na kukamilika kwa barabara hiyo kutasaidia kuongeza ajira kwa wakazi wa Msalala.
MBUNGE AOMBA BARABARA ZA MITAA ZA LAMI
Katika hatua nyingine, Mbunge wa eneo hilo ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami katika miji inayokua kwa kasi iliyopo kwenye ukanda wa Kahama–Kakola.
Ametaja Segese, Lunguya na Kakola, akisema miji hiyo imekua kwa kasi na inahitaji miundombinu ya ndani ili wananchi wanufaike kikamilifu na barabara kuu inayojengwa.
Amesema hata ujenzi wa kilomita chache za barabara za mitaa ungekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi.
UMEME WA UZALISHAJI WAOMBEWA
Mbunge huyo pia ameiomba Serikali kuhakikisha umeme unafika katika maeneo yote ya Msalala, akisisitiza kuwa mahitaji ya umeme katika eneo hilo si kwa matumizi ya majumbani pekee, bali pia kwa shughuli za uzalishaji.
Amesema baadhi ya wachimbaji bado wanatumia dizeli kuendesha shughuli zao za uchimbaji, hali inayoongeza gharama za uzalishaji.
“Jimbo hili ni jimbo la uzalishaji. Tunahitaji umeme kila mahali. Umeme wa huku si wa kuacha taa za nyumbani peke yake. Huku ni uzalishaji,” amesema.
Akijibu hoja hiyo, Ndejembi amesema Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaandaa mradi maalum wa kupeleka umeme wa kutosha katika maeneo ya uzalishaji madini, ikiwemo Shinyanga, Geita na Chunya mkoani Mbeya.
WANANCHI WATAKA USALAMA WA WANAFUNZI
Wananchi nao wameeleza matumaini yao kuhusu barabara hiyo, huku wakitaka uboreshaji wa miundombinu uende sambamba na hatua za usalama.
Fridom, mkazi wa Kahama, amesema barabara hiyo itarahisisha usafiri, lakini ameiomba Serikali kuweka alama na vibao katika maeneo ambayo wanafunzi huvuka barabara.
“Hii barabara itasaidia usafiri haraka. Naomba angalau sehemu za kupitia wanafunzi ziwekwe alama… kuwepo na vibao,” amesema.
Amesema madereva wanaweza kuongeza kasi baada ya barabara kuwa nzuri, hivyo wanafunzi wanapaswa kupewa elimu ya matumizi salama ya barabara.
MADEREVA: “CHANGAMOTO YETU ILIKUWA BARABARA”
Kwa upande wa madereva wanaofanya safari kati ya Kahama na Kakola, ubovu wa barabara umekuwa moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiathiri shughuli zao.
Mmoja wa madereva hao amesema ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ni faraja kwao na kwa wananchi wanaotumia njia hiyo.
“Changamoto zetu ilikuwa ni barabara… Asante sana, shukrani sana kwa sababu barabara yetu hii…” amesema.
BARABARA YA UCHUMI MPYA
Kwa ujumla, barabara ya Kahama–Kakola haionekani tena kama njia ya usafiri pekee, bali imeanza kutazamwa kama mhimili wa uchumi wa Kahama na Msalala.
Kukamilika kwake kunatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, kupunguza muda wa safari, kuchochea shughuli za madini na kilimo, kuongeza thamani ya maeneo ya uwekezaji na kuvutia viwanda pamoja na ajira.
Hata hivyo, ujumbe wa Waziri Ndejembi katika ziara hiyo ulikuwa mmoja: fedha zimetengwa, kazi imeanza na wananchi wanasubiri—sasa kinachotakiwa ni kuongeza kasi na kuhakikisha barabara inakamilika kwa wakati.













No comments:
Post a Comment