Na Neema Nkumbi, Kahama
MBUNGE wa jimbo la khama mjini Benjamin ngayiwa amewataka Wanasimba wa Tawi la Kagongwa kutumia umoja na mshikamano walionao kuingia katika uwekezaji mkubwa, ikiwemo kupata ardhi yenye hati na kujenga miradi itakayoliingizia tawi mapato ya kudumu pamoja na serikali.
Mbunge huyo ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Simba Day yaliyowakutanisha Wanasimba wa Tawi la Kagongwa, akisema nguvu kubwa waliyonayo kupitia umoja wao inapaswa sasa kuelekezwa katika kujenga miradi ya biashara na uwekezaji wa muda mrefu.
Amesema Wanasimba hawapaswi kubaki katika shughuli za kushabikia na kuangalia mpira pekee, bali wanapaswa kutumia umoja wao kujenga miradi itakayowanufaisha wao na jamii inayowazunguka.
Amesema hatua ya kwanza ni kupata eneo la ardhi na kulirasimisha kwa kupata hati ya umiliki, ambapo eneo hilo linaweza kutumika kujenga ofisi kubwa ya tawi, ukumbi, maduka na miradi mingine ya kibiashara.
“Msibaki kwenye ofisi tu. Muwe na eneo kubwa ambalo linaweza kuwa kituo cha uwekezaji. Mnaweza kujenga ukumbi, maduka ambayo mtapangisha watu na kupata mapato. Huo ndio uwekezaji tunaotaka kuufikia,” amesema.
Amesema uwekezaji huo unaweza kupanuliwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara, viwanda na utalii, huku akisisitiza kuwa jamii ya Kagongwa inapaswa kunufaika kupitia ajira na fursa za biashara zitakazotokana na miradi hiyo.
DIWANI MASOLWA AIPONGEZA TAWI
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kagongwa, Ismail Masolwa, amewapongeza Wanasimba wa tawi hilo kwa mshikamano na ushirikiano walioujenga, akisema hatua waliyofikia ni msingi mzuri wa kufikia malengo makubwa zaidi.
Masolwa amesema Wanasimba wa Kagongwa wameonyesha kuwa umoja unaweza kuvuka mipaka ya michezo na kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amesema tawi hilo limeendelea kuwaunganisha Wanasimba katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kushirikiana wakati wa misiba na changamoto zinazowakabili wanachama.
Diwani huyo amewataka kuendelea kudumisha umoja huo na kutumia nguvu waliyonayo katika kuanzisha miradi yenye tija kwa wanachama na wananchi wa Kagongwa kwa ujumla.
LISALA YATOA MWANGA WA MAFANIKIO YA TAWI
Akisoma, Lisala ameeleza mafanikio yaliyopatikana katika Tawi la Simba Kagongwa tangu kuanzishwa kwake, akitaja kuongezeka kwa wanachama, kuimarika kwa ushirikiano pamoja na ushiriki wa tawi katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Amesema tawi limeendelea kujenga mazingira ya kuwaunganisha Wanasimba na kuwa familia moja, huku likishirikiana na wanachama katika nyakati za furaha na changamoto.
Ameeleza kuwa hatua inayofuata ni kuhakikisha tawi linaweka mikakati madhubuti ya kujenga uwezo wake kiuchumi ili liweze kujiendesha na kutekeleza mipango yake bila kutegemea michango pekee.
Lisala hiyo imesema azma ya kuingia katika uwekezaji ni sehemu ya maono ya kulijenga Tawi la Simba Kagongwa kuwa na mali zake na vyanzo vya mapato vya kudumu.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yatahitaji ushirikiano wa viongozi, wanachama na wadau mbalimbali ili kuhakikisha mipango ya tawi inatekelezwa kwa mafanikio.
Maadhimisho ya Simba Day katika Tawi la Kagongwa yamekuwa pia fursa ya kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Wanasimba, huku viongozi wakiwahimiza kuendelea kuiunga mkono Simba Sports Club na wakati huo huo kujenga msingi wa maendeleo ya tawi lao.
No comments:
Post a Comment