Madaktari Nchini Sri Lanka wamefanya upasuaji wa kuliondoa jiwe lenye uzito wa kilo 3.1 kwenye kibofu cha mkojo cha Mwanaume mwenye umri wa miaka 55.
Upasuaji huo umefanyika katika Hospitali Kuu ya Trincomalee, Mashariki mwa Sri Lanka, baada ya Mwanaume huyo kulazwa hospitalini kufuatia kupata kiharusi ambapo Madaktari waligundua tatizo hilo baada ya kubaini kuwa alikuwa akipata changamoto wakati wa kukojoa.
Jiwe hilo lilikuwa na urefu wa takribani sentimita 17, likiwa na ukubwa unaokaribiana na yai la mbuni na uzito unaokaribiana na wa Mtoto anayezaliwa, ambapo Daktari aliyeongoza upasuaji huo, Dkt. Prahalahan Balakrishnan amesema kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, huenda likawa miongoni mwa mawe makubwa zaidi ya kibofu kuwahi kurekodiwa na kuondolewa kwa upasuaji.
Madaktari wanaamini jiwe hilo lilikuwa limejikusanya kwenye kibofu cha mgonjwa huyo kwa kipindi cha kati ya miaka mitano hadi 10, kwa sasa anaendelea kupata matibabu hospitalini kutokana na matatizo mengine ya kiafya, huku madaktari wakisema hali yake ni nzuri.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Guinness World Records, rekodi ya jiwe kubwa la kibofu lililoondolewa ilikuwa ya jiwe lenye uzito wa kilo 1.9 na urefu wa sentimita 17.9, lililoondolewa Nchini Brazil mwaka 2003 huku jiwe lililoondolewa Sri Lanka likiwa na uzito mkubwa zaidi wa kilo 3.1.
#MillardAyoUPDATES



No comments:
Post a Comment