Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda akielezea mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 katika wilaya hiyo
Na Neema Nkumbi, Kahama
Wilaya ya Kahama imeendelea kutekeleza miradi na programu mbalimbali za maendeleo katika sekta za uzalishaji, huku madini, kilimo na mifugo zikitajwa kuwa miongoni mwa sekta zinazoendelea kuchochea shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 iliyosomwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda, katika kipindi cha Novemba 2025 hadi Juni 2026, Wilaya ya Kahama imeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kutumia fedha zilizotolewa na Serikali.
Dc Nkinda amesema kwa ujumla, Kahama imepokea jumla ya Sh. 295,211,700,396.6 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika kipindi hicho.
MADINI YAZIDI KUIJENGEA KAHAMA UCHUMI
Katika sekta ya madini, taarifa inaonyesha ongezeko la utoaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo kutoka 290 hadi 1,650, hatua inayotajwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za uchimbaji.
Sambamba na hilo, makusanyo ya maduhuli ya madini yameongezeka kutoka Sh. 105,553,514,527.16 mwaka 2021/22 hadi Sh. 193,988,549,605.59 mwaka 2025/26.
Ongezeko hilo ni zaidi ya Sh. bilioni 88.4, likionyesha kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini katika mapato na shughuli za kiuchumi.
KILIMO: HUDUMA ZA UMWAGILIAJI ZABORESHWA
Katika sekta ya kilimo, Chama Cha Mapinduzi kimeeleza kuwa Serikali imeendelea kusimamia mapinduzi ya kilimo kwa kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha na salama.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kuimarisha huduma za umwagiliaji, ambapo taarifa inaeleza kuwa kuna vituo 104, vipimo vya udongo 3 na visima 96 kwa ajili ya shughuli zinazohusiana na kilimo.
Hatua hizo zinalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kuwawezesha wakulima kupata mazingira bora ya uzalishaji, hususan katika maeneo yanayohitaji huduma za umwagiliaji.
MIFUGO: DAWA ZA RUZUKU ZAWAFIKIA WAFUGAJI
Kwa upande wa mifugo, Serikali imeendelea kuimarisha ufugaji kwa kuongeza upatikanaji wa huduma za mifugo, ikiwemo dawa na chanjo.
Taarifa inaonyesha kuwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongezeka kwa usambazaji wa dawa za ruzuku, huku jumla ya lita 1,360 za dawa na dozi 427,000 za chanjo zikitajwa kutolewa kwa ajili ya kudhibiti magonjwa ya mifugo.
Hatua hiyo inalenga kupunguza madhara yanayosababishwa na magonjwa ya mifugo na kuhakikisha wafugaji wanapata huduma muhimu za kinga na tiba kwa wakati.
Hatua hizo zinaonyesha jitihada za Serikali katika kuimarisha sekta za uzalishaji na kuongeza fursa za wananchi kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Madini, kilimo na mifugo ni miongoni mwa sekta zinazogusa moja kwa moja maisha ya wananchi wa Kahama, hivyo uwekezaji katika maeneo hayo unatarajiwa kuongeza ajira, kipato cha wananchi na mapato ya Serikali.
Takwimu hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, huku Serikali ikiendelea kusisitiza matumizi ya rasilimali katika miradi inayolenga kuchochea maendeleo na kuboresha huduma kwa wananchi.



















No comments:
Post a Comment