BALOZI OMAR ASISITIZA USHIRIKIANO KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 2 August 2026

BALOZI OMAR ASISITIZA USHIRIKIANO KUCHOCHEA MAPINDUZI YA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI



Serikali imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano thabiti kati ya sekta mbalimbali ili kuongeza tija na kasi ya maendeleo katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuziwezesha sekta hizo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.



Hayo yalibainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar, wakati alipotembelea Viwanja vya Dk. John Samwel Malecela vilivyopo Nzuguni, Dodoma, ili kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo 2026.

Mheshimiwa Balozi Omar alieleza kuwa maendeleo endelevu hayawezi kupatikana endapo kila sekta itafanya kazi kwa kujitenga, akisisitiza kuwa kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda, biashara na sekta ya fedha zinapaswa kushirikiana kwa karibu ili kuongeza uzalishaji, kuchochea uchakataji wa mazao na kuimarisha huduma zinazounga mkono mnyororo mzima wa uzalishaji.

Aliongeza kuwa taasisi za kifedha zinapaswa kuendelea kuunga mkono maeneo ambayo Serikali imeyapa kipaumbele ili kuongeza kasi ya uwekezaji, sambamba na kueleza kuwa serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu matumizi ya matrekta yaliyotolewa kwa wakulima ili kuhakikisha yanatumika kama ilivyokusudiwa katika kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao.

Akizungumzia suala la masoko na utafiti, Mheshimiwa Balozi Omar aliwapongeza wajasiriamali wanaozalisha bidhaa zenye ubora lakini akasisitiza ulazima wa kuweka mikakati madhubuti ya kuzitafutia masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuongeza ushindani na mchango wake katika pato la taifa, akibainisha kuwa uwekezaji katika utangazaji wa bidhaa na uboreshaji wa mazingira ya biashara ni wa lazima.

Aliongeza kuwa utafiti ni nguzo kuu ya maendeleo ya sekta za uzalishaji, na hivyo uwekezaji mkubwa katika taasisi za utafiti kama vile Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI) ni wa msingi ili kuleta mageuzi kupitia teknolojia na ubunifu wenye tija.

Mheshimiwa Balozi Omar alihitimisha kwa kuyapongeza maandalizi na ubunifu uliodhihirishwa na washiriki katika maonesho hayo yanayokwenda sambamba na kauli mbiu ya "Tambua soko, Ongeza Tija kutekeleza Dira 2050", akionyesha kuridhishwa na jinsi maonesho hayo yalivyofanikiwa kuonyesha fursa zilizopo na kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia wadau wake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso