“WOMEN TAKING OVER” YA BARRICK YAWATIA MOYO WANAWAKE KUTOBAKI NYUMA SEKTA YA MADINI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 6 July 2026

“WOMEN TAKING OVER” YA BARRICK YAWATIA MOYO WANAWAKE KUTOBAKI NYUMA SEKTA YA MADINI


Baadhi ya wafanyakazi wanawake wa Barrick North Mara, Bulyanhulu pamoja na kampuni za wakandarasi wazawa wakiwa katika picha ya pamoja katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake katika Sekta ya Madini yaliyofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara chini ya kaulimbiu ya "Women Taking Over"
Maonyesho ya mavazi na sare mbalimbali zinazotumika migodini yalikuwa miongoni mwa vivutio vilivyopamba maadhimisho ya Siku ya Wanawake katika Sekta ya Madini.
Zoezi la kukata keki likiendelea wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake katika Sekta ya Madini, yaliyoandaliwa na Barrick North Mara chini ya kaulimbiu ya "Women Taking Over."
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake katika Sekta ya Madini yaliyofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Meneja Mahusiano Msaidizi wa Barrick North Mara, Nasieku Kisambu, akisoma risala kwa mgeni rasmi, akieleza mafanikio na shughuli mbalimbali zilizotekelezwa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake katika Sekta ya Madini yaliyofanyika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.


Baadhi ya washiriki walitunukiwa vyeti
Baadhi ya washiriki walitunukiwa vyeti
Baadhi ya washiriki walitunukiwa vyeti
Baadhi ya wanawake walioshiriki katika picha ya pamoja
Baadhi ya wanawake walioshiriki katika picha ya pamoja
Meneja Mkuu Apolinary Lyambiko akiwa na Maofisa waandamizi wa mgodi wa Barrick North Mara.


***


Katika kuendelea kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya madini, Kampuni ya Barrick imefanya maadhimisho makubwa ya Siku ya Wanawake katika Sekta ya Madini yaliyowakutanisha wafanyakazi wanawake kutoka migodi ya North Mara na Bulyanhulu pamoja na wanawake kutoka kampuni mbalimbali za wakandarasi wazawa wanaoshirikiana na migodi hiyo.


Maadhimisho hayo, yaliyofanyika katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara chini ya kaulimbiu ya "Women Taking Over", yalijumuisha shughuli za kikazi, kijamii, michezo na utoaji wa misaada, kabla ya kuhitimishwa kwa sherehe kubwa iliyowaleta pamoja wanawake hao kusherehekea mchango wao katika maendeleo ya sekta ya madini.


Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko, alisema Barrick itaendelea kutekeleza sera zinazolenga kuongeza idadi ya wanawake katika sekta ya madini kwa kuhakikisha wanapata fursa sawa za ajira, maendeleo ya taaluma na mazingira salama ya kufanyia kazi.


"Hatupo hapa tu kusherehekea tukio la wanawake, bali pia kuondoa vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini. Ushiriki wao ni sehemu ya wajibu wetu," alisema Lyambiko.


Alitoa pia wito kwa wakandarasi wote wanaofanya kazi na Barrick North Mara kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha wanawake kufanya kazi kwa usalama, heshima na ufanisi.

Awali, akisoma risala kwa mgeni rasmi, Meneja Mahusiano Msaidizi wa Barrick North Mara, Nasieku Kisambu, alisema maadhimisho hayo hayakuishia ndani ya mgodi pekee bali yalihusisha shughuli za kijamii zenye kugusa maisha ya wananchi.

Alisema wanawake hao walipata mafunzo mbalimbali ikiwemo ya usalama kazini, walitoa misaada kwa familia 60 zenye uhitaji katika vijiji vinavyozunguka mgodi wa North Mara na pia walitembelea Gereza la Wilaya ya Tarime ambako walikabidhi mahitaji muhimu kwa wafungwa na mahabusu wanawake.

Nasieku alimshukuru Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko, kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha wanawake, huku pia akiishukuru Ofisi ya Barrick Tanzania chini ya Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, kwa kuendelea kuunga mkono juhudi hizo.

Baadhi ya wanawake walioshiriki katika maadhimisho hayo walisema programu hiyo imewapa motisha mkubwa na kuonesha kuwa wanawake wana nafasi muhimu katika uzalishaji na usalama wa migodi.


Baadhi ya wanawake walioshiriki walitoa maoni yao kuhusiana na program “Hili ni jambo kubwa sana, na hii sio tu siku ya wanawake, bali nguvu ya wanawake inayoonekana kwenye uzalishaji na usalama,” alisema Zuwena Senkondo kutoka Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu ambao pia unaendeshwa na Barrick-Twiga.


Mfanyakazi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bhoke Juma kutoka kampuni ya AKO ambayo ni mkandarasi katika mgodi huo, alisema Barrick ni mfano wa kuigwa katika kujali wafanyakazi wake.


“Tungependa kuona kampuni za wakandarasi nazo zinajifunza mambo mazuri kama ambayo Barrick inawafanyia wafanyakazi wao wa kike,” alisisitiza.


Kwa upande wake, Lucy Ryoba ambaye ni mmoja wa wakandarasi wanawake katika mgodi wa North Mara, aliishukuru Barrick akisema imemfungulia milango ya fursa ya kiuchumi kwa miaka mitatu sasa.


“Barrick wanawapa wanawake kipaumbele kwenye fursa za kibiashara, inatuhamasisha kujitokeza kuchangamkia fursa za kazi za ajira na biashara mgodini,” alisema Lucy ni Mkurugenzi wa LUMRY General Supply.


Aliongeza: “Mbali na kunipa tenda za kufanya kazi mbalimbali kama vile kupamba na kutoa huduma ya chakula, Barrick wamenitangaza hadi nimeanza kupata kazi kubwa za kupamba matukio makubwa yakiwemo ya kiserikali na wanapenda kuona wanawake tunapata fursa na kuwa na mafanaiko makubwa.”


Lucy aliungana na wanawake wenzake kujipongeza kwa sherehe yao hiyo akisema imekuwa ya kihistoria, huku akishauri iwe endelevu.


Naye mfanyakazi wa mgodi wa North Mara, Neema Sokia, ambaye anaendesha mitambo katika uchimbaji madini chini ya ardhi (underground mining), alimshukuru Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko, kwa juhudi kubwa anazofanya kuhakikisha kuwa idadi ya wanawake katika mgodi huo inaendelea kuongezeka.


“Sasa hivi wanawake tuko wengi hapa North Mara japokuwa bado hatujafikia kiwango kinachotakiwa, ila General Manager (Meneja Mkuu) ametusaidia sana, tunapaza sauti tunasikika tunasikilizwa,” alisema Neema.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso