Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza katika Baraza Maalumu la Madiwani la Halmash8auri ya Msalala la kujadili hoja za CAG za mwaka wa fedha 2024/2025.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala akiwa katika Baraza Maalumu la Madiwani la
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mibako Mabubu akiwa katika Baraza Maalumu la Madiwani la
kujadili hoja za CAG za mwaka wa fedha 2024/2025
Na Neema Nkumbi, Kahama
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameiomba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalumu katika Halmashauri ya Msalala baada ya halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka, huku akieleza wasiwasi kuhusu hali ya usimamizi wa fedha na utendaji wa watumishi ndani ya taasisi hiyo.
Mhita ametoa ombi hilo wakati wa Baraza Maalumu la Madiwani la kujadili hoja za CAG za mwaka wa fedha 2024/2025, akisema hali iliyojitokeza Msalala ni ishara ya changamoto zinazohitaji kuchunguzwa kwa kina ili kubaini chanzo chake na kulinda fedha za umma.
Mbali na suala la hati yenye mashaka, RC Mhita ameeleza kuwa kumekuwepo na malalamiko ya watumishi wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria kusimamishwa au kuhamishwa bila kufuata taratibu za utumishi wa umma, jambo ambalo amesema linaweza kuchangia kushuka kwa kiwango cha utendaji wa halmashauri hiyo.
Amesema mkaguzi wa ndani wa halmashauri ana jukumu la kukagua matumizi ya fedha, kubaini mapungufu na kutoa ushauri wa kitaalamu ili kuboresha mifumo ya usimamizi wa fedha, lakini badala ya ushauri huo kuzingatiwa, kumekuwepo na mvutano unaodhoofisha kazi za ukaguzi wa ndani.
Kwa mujibu wa RC Mhita, taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa mkaguzi wa ndani aliwahi kuzuiwa kuingia ofisini kwake kwa kufungiwa mlango, huku vitasa vikidaiwa kuvunjwa na kubadilishwa, hali aliyosema haikubaliki katika ofisi za umma.
“Hata mimi Mkuu wa Mkoa siwezi kumzuia mtumishi kuingia ofisini kwa sababu si mali yangu binafsi bali ni ofisi ya serikali, Tunapofikia hatua ya kuwazuia watumishi kutekeleza majukumu yao, tunatoka nje ya misingi ya utumishi wa umma,” amesema Mhita.
Aidha, amesema pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kupitia Katibu Mkuu wake kuagiza mkaguzi huyo wa ndani asihamishwe na aendelee na kazi zake katika halmashauri hiyo, maelekezo hayo yalidaiwa kutotekelezwa.
Mhita amesema kutokutekelezwa kwa maelekezo ya wizara pamoja na ushauri kutoka kwa wataalamu mbalimbali kumeibua maswali mengi kuhusu mazingira ya utendaji ndani ya halmashauri hiyo na uwezekano wa kuwepo kwa changamoto katika mifumo ya udhibiti wa fedha.
Katika hali iliyoibua mjadala zaidi wakati wa kikao hicho, RC Mhita ametaka kufahamu alipo mkaguzi wa ndani aliyekuwa ameagizwa kubaki Msalala, Hata hivyo, mtu mmoja alisimama na kujitambulisha kuwa ndiye mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo, lakini Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama (DAS), Glory Absalum, alieleza kutomtambua kama mkaguzi husika.
Tukio hilo lilimghadhabisha Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alihoji uhalali wa hatua zilizochukuliwa dhidi ya mkaguzi wa ndani aliyekuwa akisimamia udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.
Amesema mazingira hayo yanaongeza umuhimu wa kufanyika kwa ukaguzi maalumu utakaochunguza kwa kina mfumo wa usimamizi wa fedha, utekelezaji wa maelekezo ya mamlaka za juu na changamoto zilizochangia halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka.
“Nadhani kuna kila sababu ya kuomba halmashauri hii ipate ukaguzi maalumu ili tujue changamoto iko wapi na hatua stahiki zichukuliwe kwa maslahi ya wananchi,” amesema Mhita.
Amesisitiza kuwa lengo la ukaguzi huo si kumlenga mtu binafsi bali kuhakikisha fedha zote zinazotolewa na serikali kwa ajili ya maendeleo zinawafikia wananchi na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Pia amewataka madiwani wa Halmashauri ya Msalala kuepuka migawanyiko na badala yake kutumia nafasi zao kusimamia matumizi ya fedha za umma kwa kuuliza maswali na kufuatilia utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala, Mibako Mabubu, amekiri kutoridhishwa na hali iliyopelekea halmashauri hiyo kupata hati yenye mashaka, akieleza kuwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013 haijawahi kupata hati ya aina hiyo.
Amesema baadhi ya hoja zilizochangia hati hiyo zinatokana na kutokuwepo kwa nyaraka muhimu na kuahidi kuwa uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na watendaji utahakikisha nyaraka hizo zinapatikana na hoja zilizobainishwa zinafanyiwa kazi.
Naye Diwani wa Kata ya Bulyanhulu, Musingi Sebaganga, amesema ukaguzi maalumu unaweza kusaidia kubaini chanzo halisi cha changamoto zilizopo na kuweka msingi mzuri wa kuboresha usimamizi wa fedha kwa manufaa ya wananchi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha rasilimali za umma zinalindwa, miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati na huduma zinazokusudiwa kuwafikia wananchi zinatolewa kwa ufanisi zaidi.

















No comments:
Post a Comment