
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekipongeza Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar kwa kufanya mazungumzo na kufikia maridhiano, akitaja hatua hiyo kuwa ni muhimu katika kuimarisha amani, umoja, na mshikamano nchini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rais Samia ameeleza kuwa maridhiano hayo si ishara ya udhaifu, bali ni alama ya ukomavu wa kisiasa unaoweka mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi ya vyama au ya mtu binafsi.
"Wananchi hawahitaji vurugu wala mivutano ya kisiasa isiyoisha. Wanahitaji amani, usalama, huduma bora za kijamii, ukuaji wa fursa za kiuchumi na ajira," amesema Rais Samia na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kusimama imara kulinda usalama wa raia na mali zao.
Katika kuonyesha uzito wa hatua hiyo, Mkuu huyo wa Nchi amerejea mafundisho ya vitabu vitakatifu kuhusu umuhimu wa kupatana, akitaja mstari wa Qur'ani Tukufu (Sura Al-Hujurat 10) na ule wa Biblia Takatifu (Mathayo 5:9) yanayohimiza amani na udugu miongoni mwa wanajamii.
No comments:
Post a Comment