Wananchi wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha wamehimizwa kusimama kidete kulinda na kudumisha amani pamoja na mshikamano wa kitaifa kwani ndiyo nguzo kuu inayowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa jamii nzima.
Wito huo umetolewa na mmoja wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa wa mwaka 2026, Mussa Othman Ali, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliogusa ukaguzi wa miradi ambapo alibainisha kuwa ujumbe wa mbio hizo unasisitiza mshikamano wa dhati chini ya kaulimbiu inayowakumbusha Watanzania kuwa nchi hii ni yao sote na wanapaswa kuungana kuleta maendeleo.
Kiongozi huyo alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika jitihada zake za kuwaletea maendeleo, huku akigusia masuala mtambuka ikiwemo umuhimu wa lishe bora, matumizi ya vyandarua kujikinga na malaria, kupima VVU mapema, pamoja na kushiriki kikamilifu kupiga vita rushwa na biashara ya dawa za kulevya ili kulinda nguvu kazi ya taifa.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Mondu3li, Isack Copriano, alimpongeza Mkuu wa Nchi kwa uwekezaji mkubwa wa kifedha uliowezesha ujenzi wa miundombinu ikiwemo ukamilishaji wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Migungani One, mradi unaoongozwa na Mkuu wa Shule Paulina Rasirasi ukiwa na lengo la kujiandaa mapema kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2028 na kuongeza fursa za elimu bora wilayani humo.

No comments:
Post a Comment