Na Neema Nkumbi, Kahama
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamshikilia Shukuru Bizire (38) kwa tuhuma za kumuua mkewe, Neema John (32), katika tukio linalodaiwa kutokea Julai 3, 2026, majira ya saa 10 jioni katika Mtaa wa Mwime, Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kuwa mwanaume mmoja alikuwa amemfungia ndani mke wake na kuendelea kumpiga kwa muda mrefu.
"Askari walifika katika eneo la tukio na kumkuta Neema John akiwa ndani ya nyumba akiwa amejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake," amesema Kamanda Magomi.
Amesema Shukuru Bizire anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya uchunguzi, na kwamba upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
Kamanda Magomi amesema Jeshi la Polisi linakemea vikali vitendo vya mauaji vinavyotokana na migogoro ya kifamilia na kusisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kuhusika na uhalifu wa aina hiyo.
Akizungumzia kilichotangulia kabla ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwime, Stella Bayugile, amesema siku ya tukio marehemu alikuwa kanisani kabla ya kurejea nyumbani, ambako alikuta mpangilio wa vitu ukiwa umebadilika na fedha alizokuwa akizitunza kwa ajili ya ujenzi zikiwa hazipo.
Kwa mujibu wa Bayugile, Neema alirejea kanisani kuwaaga wenzake na kueleza kuwa anakwenda kumtafuta mumewe ili kufahamu zilipo fedha hizo. Baadaye alikwenda nyumbani kwa mke mwenza wa mume wake lakini hakumkuta, huku majirani wakimweleza kuwa Shukuru alikuwa ametoka kumsindikiza mke huyo aliyekuwa akisafiri.
Amesema Neema aliamua kumsubiri mumewe na aliporejea nyumbani alimfuata ndani, ambapo walizozana. Muda mfupi baadaye kelele za kuomba msaada zilisikika kutoka ndani ya nyumba, lakini majirani hawakuweza kuingia kwa kuwa mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani.
Bayugile amesema baada ya kelele hizo kukoma, majirani walidhani wanandoa hao walikuwa wamepatana. Hata hivyo, Kamanda wa Sungusungu alipofika na kugonga mlango, Shukuru aliufungua na walikuta damu nyingi ndani ya nyumba, huku Neema akiwa tayari amefariki dunia na mwili wake ukiwa umefunikwa kwa shuka kitandani.
Amesema majeraha aliyokuwa nayo marehemu yanaashiria ukatili mkubwa, akidai alijeruhiwa kwa kitu kinachodhaniwa kuwa na ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mwili wa Neema John umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi, huku Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

No comments:
Post a Comment