VIJIJI 9 MSALALA VYAJIPANGA KUWA VYA KISASA: MAENEO YA HUDUMA YAAINISHWA KUPITIA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 19 June 2026

VIJIJI 9 MSALALA VYAJIPANGA KUWA VYA KISASA: MAENEO YA HUDUMA YAAINISHWA KUPITIA MPANGO WA MATUMIZI BORA YA ARDHI

  



Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kashishi kata ya Kashishi Halmashauri ya Msalala, mkoani Shinyanga wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kijiji hicho uliokuwa na lengo la kupitisha sheria ndogo zitakazoongoza mpango wa matumizi ya ardhi kwa kipindi cha miaka 10, 2026-2036.


Na Mwandishi wetu, Msalala-Shinyanga


Wananchi wa vijiji 9 vya halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kikiwemo cha Kashishi, wameeleza furaha yao kubwa baada ya kufikiwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, wakisema mradi huo utaleta maendeleo makubwa kijijini kwao.



Akizungumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Rozi Daudi Jegu alisema walipokea mradi huo kwa mikono miwili. “Kwa kweli sisi wanakijiji wa Kashishi tumefurahi sana kupokea huu mradi. Tumeupokea kwa furaha sana, kwa sababu huu mradi unaonekana utatuletea maendeleo katika kijiji chetu,” alisema Rozi.



Amesema “Tulikuwa hatujawahi kuletewa elimu ya matumizi ya ardhi. Lakini kwa sasa hivi tumepewa elimu, tumeipokea vizuri. Huu mradi tunajua unatupeleka vizuri.”



Aliongeza kuwa tayari wameanza kuona faida zake. Kutokana na hilo, wanakijiji wanaomba mradi uendelee. “Tunaomba sisi kama wanakijiji cha Kashishi, huu mradi usiishie ili tuweze kupata hizo huduma nzuri.”



Naye Ramazani Madesa, mkazi wa Kashishi, amesema mradi wa makazi bora umepokelewa vizuri. “Tunafurahi kwa sababu hii kata inakuwa sasa. Tumekuwa tukijenga kiholela-holela, na sasa hivi tumepokea elimu, waharakishe mradi uje tupate huduma za kijamii karibu.”



Amesema elimu waliyopata itasaidia kupunguza migogoro. “Haitakuwa na migogoro ya ardhi kwa sababu watu wanaelewa na wanajua mipaka yao. Viongozi wetu wanajua hatua za kuchukua.”



Hata hivyo wananchi wa Kashishi wanaamini mradi huo utabadilisha sura ya kata yao. “Kata itakuwa na majengo ya kisasa. Itakuwa nzuri, itakuwa na majengo safi na wananchi watanufaika. Pili, hata migogoro ya kugombea maeneo haitakuwepo kwa sababu yote imepangwa.”



Aidha ameushukuru uongozi wa kijiji kwa ushirikiano, kutokana na wao kufanya kazi hiyo kwa umoja na viongozi kijiji, huku wakitarajia maendeleo makubwa ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.



Wananchi hao wameiomba serikali na wadau kuendeleza mradi huo ili maeneo yote ya kijiji yapangwe. “Tunawaomba wakabidhi maeneo yaliyobaki yapangwe. Tunataka Kashishi yote ipangike ili kila mwananchi anufaike,” alihitimisha Rozi.



Mradi wa matumizi bora ya ardhi unalenga kupanga vijiji ili kuondoa migogoro, kurahisisha upatikanaji wa huduma, na kuchochea uwekezaji wa kisasa vijijini, ambapo katika halmashauri ya Msalala vijiji 9 vimefikiwa na mpango huo.



Mwenyekiti wa Kijiji cha Kashishi, Marco Ligwa, amesema mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya kijiji hicho, na kwamba Kashishi inakwenda kuanza safari ya mageuzi makubwa yanayolenga kukibadilisha na kuwa kijiji cha kisasa.



"Mpango huu utasaidia kukipanga kijiji chetu kisasa kabisa. Huduma za jamii zitawafikia wananchi kwa urahisi zaidi, na muhimu zaidi utapunguza migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikitukwaza kwa muda mrefu," amesema Ligwa.



Ligwa ameongeza kuwa tayari hatua kubwa imepigwa, ambapo maeneo ya huduma mbalimbali yameainishwa. Miongoni mwa maeneo hayo ni eneo la uwekezaji, eneo maalum la malalo ambalo awali halikuwepo kijijini hapo, eneo la soko la kisasa, pamoja na kutengwa kwa eneo la kituo cha mabasi.



Kwa upande wake, Anthony Maganga kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Kanda ya Ziwa, amefafanua kuwa zoezi lililofanyika leo ni la utambulisho wa sheria ndogo.



"Shughuli iliyofanyika leo ni utambulisho wa sheria ndogo zitakazoongoza mpango huu wa matumizi bora ya ardhi kwa kipindi cha miaka 10 ijayo," amesema Maganga.



Mpango huu unatajwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa Kashishi, ikiwa ni pamoja na kuongeza thamani ya ardhi, kuvutia wawekezaji, na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa urahisi.














No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso