Na Beda Msimbe, TBN, St. Petersburg
Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, amesema Tanzania ni lango muhimu la kimkakati linalounganisha soko la Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa, huku akiitaja kuwa miongoni mwa mataifa yenye nafasi kubwa katika uchumi wa dunia unaoendelea kubadilika.
Akizungumza Juni 5, 2026 katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026), Rais Putin alisema Tanzania ina nafasi ya kipekee kutokana na eneo lake la kijiografia na mchango wake katika kuunganisha biashara za kikanda na za kimataifa.
Alifananisha nafasi ya Tanzania katika Afrika Mashariki na ile ya Uzbekistan katika ukanda wa Asia ya Kati, akieleza kuwa mataifa hayo yanatumika kama viungo muhimu kati ya uchumi wa kikanda na vituo vikuu vya biashara duniani.
“Mataifa yenye uwezo wa kuoanisha maendeleo yao ya ndani na miunganisho madhubuti ya biashara na uchumi wa kimataifa yanaendelea kuwa na umuhimu mkubwa kadri mfumo wa uchumi wa dunia unavyozidi kubadilika,” alisema Putin.
Rais huyo alibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayonufaika na nafasi yake ya kijiografia pamoja na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya usafiri na biashara, jambo linaloongeza ushindani wake katika soko la kimataifa.
Kauli za Putin zinakuja wakati Tanzania ikiendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo bandari, reli na njia za usafirishaji zinazolenga kuifanya nchi kuwa kitovu kikuu cha biashara na usafirishaji kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Katika jukwaa hilo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipata fursa ya kuelezea mazingira ya uwekezaji na biashara nchini pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali katika kukuza uchumi na kuvutia wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali.
Rais Samia alisema Tanzania ipo tayari kushirikiana na nchi yoyote yenye nia njema ya kuchangia maendeleo ya wananchi wake kupitia uwekezaji, biashara, teknolojia na ushirikiano wa kiuchumi.
Akijibu swali kuhusu ushirikiano na Urusi katika mazingira ya vikwazo vya kimataifa, Rais Samia alisema Tanzania inaendelea kufanya kazi na washirika wote wanaoitakia mema nchi yake bila ubaguzi.
“Tanzania haina vikwazo. Tunafanya kazi na washirika wote wanaoitakia mema nchi yetu na wanaotaka kushirikiana nasi katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu,” alisema Rais Samia.
Kauli za viongozi hao zinaashiria kuendelea kuimarika kwa mahusiano ya Tanzania na Urusi pamoja na kuongezeka kwa fursa za ushirikiano wa kiuchumi, biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.


No comments:
Post a Comment