MIAKA 30 YA TRA, MKOA WA KAHAMA WAKUSANYA ZAIDI YA 120% KWA MWAKA 2025/2026, YAFANYA JOGGING NA KUPANDA MITI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 27 June 2026

MIAKA 30 YA TRA, MKOA WA KAHAMA WAKUSANYA ZAIDI YA 120% KWA MWAKA 2025/2026, YAFANYA JOGGING NA KUPANDA MITI



Watumishi wa TRA mkoa wa kikodi Kahama, walipa kodi na wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo Kahama Jogging Club, katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa shughuli ya Jogging, ikiwa ni kuadhimisha miaka 30 ya Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), sambamba na kuwahamasisha .jamii kuhusu umuhimu wa ulipaji wa kodi kwa hiari.



Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoa wa kikodi Kahama, Wisaka Kamwamu (kulia) akipanda mti katika shule ya sekondari Kishimba iliyopo Manispaa ya Kahama, ikiwa ni kuadhimisha miaka 30 ya TRA, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali za kuhifadhi mazingira sambamba na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa ulipaji wa kodi kwa hiari.



📍KAHAMA


Katika kuadhimisha miaka 30 ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Mamlaka hiyo katika Mkoa wa Kikodi Kahama, imevuka lengo la makusanyo ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 44, sawa na zaidi ya asilimia 120 ya lengo la Shilingi bilioni 35.



TRA mkoa wa Kahama unaadhimisha miongo hiyo mitatu kwa shughuli mbalimbali zilizohusisha walipa kodi waliopo sambamba na kuwatengeneza wapya, ikiwemo mazoezi ya pamoja (jogging) pamoja na upandaji wa miti.


Meneja wa TRA mkoa wa Kahama, Wisaka Kamwamu, akizungumza mara baada ya kumalizika kwa shughuli ya jogging, ametaja chanzo cha mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ushirikiano mzuri kati ya TRA, walipa kodi na viongozi wa serikali kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kahama.


Jogging hiyo iliyowakutanisha watumishi wa TRA, walipa kodi na wadau mbalimbali wa michezo, wakiwemo Kahama Jogging Club, Kamwamu amesema tukio hilo limelenga kuwapongeza walipa kodi kwa mchango wao katika maendeleo ya Taifa na kuimarisha uhusiano kati ya TRA na wadau wake.


Amesema tangu kuanzishwa kwa TRA, taasisi hiyo imeendelea kupitia hatua mbalimbali za maboresho, huku kipindi cha miaka ya hivi karibuni kikishuhudia ongezeko kubwa la makusanyo katika Mkoa wa Kahama.


Amesema "Lengo letu la siku hii ni kutambua mchango wa walipa kodi wetu, na namna ambavyo tumeshirikiana nao katika hatua mbalimbali za kikodi. Ushirikiano huu umetupa mafanikio makubwa kwenye makusanyo.”



Amesema mwitikio mkubwa wa wafanyabiashara, wanamichezo na wananchi katika jogging hiyo, umeongeza hamasa kwa watumishi wa TRA na walipa kodi, jambo litakaloendelea kuimarisha uhusiano na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.


Kwa mujibu wa Kamwamu, katika mwaka wa fedha unaomalizika, TRA Kahama ilipangiwa kukusanya Shilingi bilioni 35, lakini hadi sasa imefanikiwa kukusanya zaidi ya Shilingi bilioni 44, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Shilingi bilioni 9.


Amesema hayo ni mafanikio makubwa ambayo yameifanya Kahama kuendelea kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika makusanyo kwa miaka mitatu mfululizo.


Kamwamu ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya watumishi wa TRA, wafanyabiashara, viongozi wa serikali pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali, ambayo imerahisisha huduma nyingi za kikodi bila ulazima wa walipa kodi kufika katika ofisi za TRA.


Aidha, aliwataka wafanyabiashara kuendelea kushirikiana na TRA kwa kufika katika ofisi zake kila wanapokutana na changamoto ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.



"TRA ni chombo cha wananchi. Bila ushirikiano wa walipa kodi hatuwezi kufikia malengo yetu ya ukusanyaji wa mapato. Tunawaomba waendelee kushirikiana nasi ili tuendelee kujenga uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla," ameongeza


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kahama Jogging Club, Abdallah Mmagane, amesema ushirikiano kati ya klabu hiyo na TRA umekuwa wa mfano, na umewezesha wananchi wengi kushiriki mazoezi yanayolenga kuboresha afya na kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.


Amesema Kahama Jogging Club itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, katika kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi kwa ajili ya afya bora.


Naye Afisa Habari wa Kahama Jogging Club, Ketty Rugy, amesema wamewiwa kushiriki maadhimisho ya miaka 30 ya TRA kwani wanachama wengi wa klabu hiyo ni wafanyabiashara, huku akiwasihi kuendelea kulipa kodi kwa hiari.


Amesema "Tumeshiriki wengi kwa sababu wengi wetu ni wafanyabiashara, hivyo tumekuwa tukishirikiana kwa karibu sana na TRA. Ninawaomba wafanyabiashara wote tuendelee kulipa kodi, bila kodi hakuna maendeleo ya nchi yetu."


Wakati huohuo TRA Mkoa wa Kikodi Kahama, imepanda miti katika Shule ya Sekondari Kishimba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA, na kutekeleza wajibu wake kwa jamii (Corporate Social Responsibility), mara baada ya kumalizika kwa shughuli ya.


Meneja Kamwamu amesema shule hiyo imechaguliwa kwa makusudi kutokana na nafasi yake ya kulea kizazi kitakachokuwa walipa kodi na wataalamu wa baadaye, wakiwemo maofisa wa kodi.


Amesema "Tumekuja Kishimba sekondari kwa sababu tunatambua hapa ndipo wanalelewa vijana wetu. Hawa ndiyo walipa kodi wa kesho na tunategemea pia kupata maofisa wa kodi. Hii ni sehemu ya wajibu wetu kwa jamii kama taasisi ya serikali.”


Aliongeza kuwa walimu wa shule hiyo pia ni walipa kodi wanaochangia mapato ya serikali, hivyo TRA itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu katika kuhamasisha maendeleo na utunzaji wa mazingira.


Naye Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kishimba, Adelina Massawe, ameishukuru TRA kwa kuichagua shule hiyo, na kwamba miti hiyo itachangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa kutunza mazingira.


"Tunawashukuru sana TRA kwa kutuchagua, huu ni ujumbe mzuri kwa wanafunzi wetu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira. Miti hii itasaidia kuboresha mazingira ya shule na kuwapa wanafunzi sehemu nzuri za kujifunzia na kufanya majadiliano.” Amesema Massawe





















No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso