Katibu tawala wilaya ya Kahama Glory Absalum akishuhudia mashindano ya mpira wa miguu kati ya watumishi wa afya na idara ya elimu sekondari katika kuhitimisha mashindano ya KMC watumishi Cup 2026 katika uwanja wa Taifa , Kahama.
Katibu tawala wilaya ya Kahama Glory Absalum akimkabidhi tuzo ya mchezaji mwenye hamasa, mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu, kwenye fainali za mashindano ya KMC Watumishi Cup 2026 yaliyofanyika katika uwanja wa Taifa, Kahama.
Na Neema Nkumbi - Kahama, Shinyanga
Baada ya mwezi mzima wa ushindani, burudani na kujenga afya miongoni mwa watumishi wa umma katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, mashindano ya KMC Watumishi Cup 2026 yamehitimishwa rasmi Juni 5, 2026 katika Uwanja wa Taifa Kahama, yakihusisha watumishi kutoka idara mbalimbali za Serikali ndani ya Manispaa hiyo.
Mashindano hayo yaliyoanza Mei 5, 2026, yalilenga kuimarisha afya za watumishi, kujenga ushirikiano mahali pa kazi pamoja na kuibua vipaji vya michezo vinavyoweza kuwakilisha Manispaa katika mashindano mbalimbali ya kitaifa.
Mgeni maalum katika mashindano hayo ambaye ni katibu tawala wa wilaya ya Kahama Glory Absalum amemwagiza mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu kuandaa vilabu mbalimbali vya michezo ili kuimarisha afya za watumishi.
Ameipongeza halmashauri kwa mashindano hayo yanayoibua ari mpya kazini, ushirikiano baina ya watumishi, huku akisisitiza watumishi kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia heshima, taratibu na miongozo ya kazi.
“Nikupongeze sana mkurugenzi, ni wachache sana wanaothubutu kukifanya hiki ulichokifanya, tumeona watumishi wote wameweza kujumuika na kufanya kinachotakiwa, yote haya ni juhudi zako mkurugenzi, hongera sana.” Amesema Absalum
Aidha amesema kila kata inatakiwa kuanzisha vikundi vya mazoezi kuendelea kutunza afya za watumishi, ushirikiano na mshikamano miongoni mwao.
“Wengi hatufanyi mazoezi, unatoka asubuhi na gari unaenda ofisini ukimaliza unapanda gari unarudi nyumbani. Tumepanga hapa tuwe na mazoezi ya kila wiki, mkurugenzi na mimi nitajitahidi kuhudhuria, tuondokane na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.”
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amekiri kupokea maelekezo hayo na kuahidi kuyatekeleza kwa wakati.
Amewapongeza watumishi wote walioshiriki mashindano hayo kwa kuonyesha nidhamu, ushindani wa kirafiki na mshikamano mkubwa tangu kuanza hadi kufikia hatua ya mwisho.
Kibetu amesema lengo la michezo hiyo ni kujenga umoja na mahusiano mazuri miongoni mwa watumishi, jambo ambalo huongeza ari ya kufanya kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi wao.
Amebainisha kuwa mafanikio ya KMC Watumishi Cup 2026 yanaonyesha dhamira ya Manispaa ya Kahama ya kuendelea kuwekeza katika michezo na ustawi wa watumishi wake, huku akitoa wito kwa washiriki kuendeleza ari ya ushirikiano waliyoionyesha wakati wote wa mashindano.
“Ushindani ulikuwa mkubwa kwelikweli na kila mmoja alihitaji ushindi unaoonekana. Niseme tumepokea maelekezo, ushauri na tutaufanyia kazi, lakini watumishi tujitahidi kufanya mazoezi.” Amesema Kibetu na kuongeza
“Lerngo haswa ni kuleta mshikamano kwa watumishi ili kuleta maendeleo kwa Kahama na Tanzania, watumishi kufanya mazoezi, na pia ni maandalizi ya kupata wachezaji wapya watakaoshiriki mashindano ya shirikisho la michezo serikali za mitaa (SHIMISEMITA).”
Awali akitoa taarifa ya mashindano ya KMC watumishi Cup 2026, afisa Michezo wa Manispaa ya Kahama, Martha Kapela alisema KMC Watumishi Cup 2026, imekuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha watumishi kutoka idara tofauti na kuwapa nafasi ya kushiriki shughuli za michezo sambamba na majukumu yao ya kila siku.
Kapela aamesema mashindano hayo yaliyoanza Mei 5 na kutamatika Juni 5, 2026, yameshirikisha watumishi 4,376 kutoka idara zote za Manispaa ya Kahama, na mashindano yalifanyika nje ya saa za kazi.
Ametaja michezo iliyoshoindaniwa kuwa ni pamoja na mpira wa miguu, netball, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa mikono, riadha, pool table, karata, bao kula na kunywa, kuvuta kamba, drafti, darts, ucheshi, kwaya, ngoma na bongo fleva.
Amesema “Kwa siku ya leo, michezo iliyoshindaniwa ni mpra wa miguu kati ya watumishi wa Afya na idara ya elimu sekondari, Netiboli ni kati ya Elimu msingi na Elimu sekondari huku riadha mita 100 ikiwa ni wanawake na wanaume kutoka idara zote."
Katibu tawala wilaya ya Kahama Glory Absalum wa kwanza kushoto akishuhudia fainali za mashindano ya watumishi Cup 2026, wa katikati ni mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama Masudi Kibetu pamoja na mwenyekiti wa chama cha mpira wa miguu wilaya ya Kahama (KDFA) Salum Hussein.
Katibu tawala wilaya ya Kahama Glory Absalum akisalimiana na timu ya mpira wa miguu ya idara ya elimu sekondari iliyoingia fainali za mashindano ya KMC Watumishi Cup 2026 ikichuana na timu ya watumishi wa idara ya afya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.






































No comments:
Post a Comment