WANANCHI WAASWA KUFANYA MIKATABA YA ARDHI KWA MAANDISHI KUEPUKA MIGOGORO
Na Neema Nkumbi, MSALALA
Wananchi wametakiwa kuhakikisha mikataba yote ya ardhi ikiwemo ununuzi wa mashamba na viwanja inafanyika kwa maandishi ili kupunguza migogoro ya ardhi inayojitokeza katika jamii.
Rai hiyo imetolewa wakati wa utoaji wa elimu ya msaada wa kisheria ya Samia Legal Aid iliyofanyika katika Kata ya Bulige, Halmashauri ya Msalala ambapo wananchi walipata nafasi ya kufahamu haki zao pamoja na taratibu sahihi za kushughulikia migogoro ya ardhi.
Afisa Ardhi wa Halmashauri hiyo, Benedictor Maganga, amesema serikali kupitia kampeni za msaada wa kisheria inalenga kuwajengea wananchi uelewa wa namna ya kutatua changamoto mbalimbali za ardhi na kujua sehemu sahihi za kuwasilisha malalamiko yao wanapokutana na matatizo.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakifanya mikataba kwa maelewano ya mdomo bila kuwa na nyaraka rasmi jambo ambalo limekuwa chanzo cha migogoro mingi katika jamii.
“Kuanzia sasa hivi umepata elimu hii, kila kitu unachofanya hasa biashara iwe kununua kiwanja au shamba ni lazima kiwe kwenye maandishi, hilo litakusaidia wewe na familia yako na kupunguza migogoro,” amesema Maganga.
Aidha, ameeleza kuwa uthibitisho wa umiliki wa ardhi hutegemea ushahidi mbalimbali ikiwemo barua za serikali za mitaa, ushahidi wa majirani pamoja na taarifa za viongozi wa eneo husika.
Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mkutano huo wameeleza changamoto wanazokutana nazo katika masuala ya ardhi na urithi huku wakiiomba serikali kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa jamii.
Mmoja wa wananchi hao, Tabitha Bunzali, amesema alinunua shamba akiwa anaishi Shinyanga Vijijini kabla ya kuhamia Msalala pia anaeneo lingine msalala lakini hadi sasa hajafanikiwa kupata hati miliki ya maeneo hayo, je anaweza kupata hati moja?, amehoji.
Kwa upande wake, Rose Daud ameomba ufafanuzi wa kisheria kuhusu haki ya urithi wa ardhi ya familia baada ya baba yake kufariki dunia na kuacha watoto saba, huku kukiishi maeneo tofauti tofauti na kuachwa yeye kama msimamizi wa eneo hilo je anaweza kupewa hati kwa niaba ya ndugu zake?, amehoji.
Wananchi wamehimizwa kufuata taratibu zote za kisheria na kutumia wataalamu katika kufanya mikataba ya ardhi ili kujiepusha na hasara pamoja na migogoro isiyo ya lazima.
No comments:
Post a Comment