WANANCHI KAHAMA WANUFAIKA NA KAMPENI YA SAMIA LEGAL AIDS, ELIMU YA ARDHI YAPEWA KIPAUMBELE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 20 May 2026

WANANCHI KAHAMA WANUFAIKA NA KAMPENI YA SAMIA LEGAL AIDS, ELIMU YA ARDHI YAPEWA KIPAUMBELE

Na Neema Nkumbi, Kahama

Wananchi wa Manispaa ya Kahama wameendelea kunufaika na huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Samia Legal Aid, huku elimu kuhusu umiliki halali wa ardhi na umuhimu wa hati miliki ikipewa kipaumbele katika siku ya mwisho ya kampeni hiyo.

Miongoni mwa wananchi walionufaika ni Peter Burilo ambaye amesema kampeni hiyo imemuwezesha kupata hati za viwanja vitatu kwa haraka bila gharama kubwa, licha ya kuwa moja ya viwanja hivyo bado lina mgogoro wa umiliki ambao unaendelea kufuatiliwa kisheria.

Burilo amesema awali yeye pamoja na wenzake walinunua eneo kabla ya mpango mji kufika katika maeneo yao, lakini baadaye serikali ilianza taratibu za upangaji wa mji zilizohusisha upimaji wa maeneo hayo. Amesema msaada wa kisheria alioupata umempa matumaini ya kupata haki yake katika mgogoro unaoendelea.

“Nina imani kupitia msaada huu wa kisheria haki yangu nitaipata,” amesema Burilo huku akiishauri serikali kuongeza muda wa utoaji wa huduma hizo ili wananchi wengi zaidi waweze kufikiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakato, Hussein Mwita, amewataka wananchi kuhakikisha wanahakiki historia ya maeneo wanayotaka kununua kupitia serikali za mitaa na majirani kabla ya kufanya manunuzi ili kuepuka migogoro ya ardhi inayoweza kujitokeza baadaye.

Mwita amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakinunua maeneo kwa maelezo ya madalali bila kufanya uchunguzi wa kina, hali inayochangia kuibuka kwa migogoro mingi ya umiliki wa ardhi licha ya maeneo mengi ya Kahama tayari kupimwa rasmi.

Naye Msajili Msaidizi wa Hati za Ardhi kutoka Mkoa wa Shinyanga, Emanuel Steven, amesema changamoto kubwa inayowakabili wananchi wengi ni ukosefu wa uelewa kuhusu umuhimu wa hati miliki pamoja na kukosekana kwa nyaraka muhimu za kisheria kama mikataba ya mauziano ya ardhi.

Amesema katika kampeni hiyo zaidi ya hati 400 za ardhi zimetolewa kwa wananchi waliofanikiwa kukamilisha taratibu za umiliki, huku wanawake wakiongoza kwa kujitokeza kunufaika na huduma hizo ambapo takribani asilimia 60 ya waliojitokeza ni wanawake na asilimia 40 ni wanaume.

Emanuel amesema mwitikio huo unaonyesha ongezeko la uelewa kwa wanawake kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi kihalali, huku akisisitiza bado kuna haja kubwa ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kufahamu taratibu sahihi za umiliki wa ardhi na umuhimu wa kuwa na nyaraka za kisheria.

Akizungumzia mgogoro wa kiwanja unaowahusisha Samuel Sitta na Peter Burilo, Mratibu wa Kampeni ya Samia Legal Aids kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Anthony Elias, amesema serikali itaendelea kufanya uchunguzi wa kina kupitia nyaraka na taratibu zote za umiliki ili kuhakikisha mwenye haki anapatiwa haki yake kwa mujibu wa sheria.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso