WAKURUGENZI WA HALMASHAURI ZA WILAYA YA KAHAMA WAAGIZWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI WA MADENI YA MAJI KATIKA TAASISI ZA UMMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 26 May 2026

WAKURUGENZI WA HALMASHAURI ZA WILAYA YA KAHAMA WAAGIZWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI WA MADENI YA MAJI KATIKA TAASISI ZA UMMA


Na Neema Nkumbi, Kahama
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amewaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote wilayani humo kufuatilia na kusimamia taasisi zinazodaiwa ankara za maji ili kuhakikisha zinalipa madeni yao kwa wakati na kuimarisha utoaji wa huduma za maji vijijini.

Agizo hilo amelitoa leo may 26, 2026 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wilaya wa Vyombo vya Kutoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO) ulioandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na kufanyika katika Manispaa ya Kahama.

Nkinda amesema taasisi nyingi za serikali pamoja na baadhi ya watu binafsi wanadaiwa ankara za maji za muda mrefu, hali inayochangia kupungua kwa mapato na kuathiri ufanisi wa utoaji wa huduma za maji kwa wananchi.

"Zipo taasisi nyingi ambazo zina madeni makubwa ya maji hivyo Nawaagiza wakurugenzi kusimamia taasisi hizo na kuhakikisha zinalipa ankara za maji kwa wakati, jambo ambalo litasaidia kuboresha utoaji wa huduma za maji kwa wananchi," amesema Nkinda.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameitaka RUWASA Kahama kuwasilisha orodha ya taasisi zote za serikali pamoja na watu binafsi wanaodaiwa ili hatua za kufuatilia na kukusanya madeni hayo zichukuliwe haraka.

"Nimesikia katika hotuba yenu kuwa taasisi nyingi za serikali pamoja na watu binafsi zina madeni ya maji, Meneja wa RUWASA Kahama nipatie orodha ya wadaiwa wote ili tufanye ufuatiliaji na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa haraka," ameongeza.

Akitoa taarifa ya hali ya utoaji wa huduma za maji wilayani Kahama, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kahama, Mhandisi Magili Maduhu, amesema wakala huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo baadhi ya watumiaji kutolipa ankara za maji kwa wakati pamoja na baadhi ya CBWSO kukosa vitendea kazi vya kutosha.

"Tunakutana na changamoto ya baadhi ya wateja kutolipa ankara za maji kwa wakati na baadhi ya CBWSO kuwa na uhaba wa vitendea kazi. Hata hivyo, tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufunga mita za malipo kabla ili watumiaji walipe kabla ya kutumia huduma ya maji," amesema Mhandisi Maduhu.

Kwa mujibu wa RUWASA, kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Wilaya ya Kahama ni asilimia 68.8, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ina asilimia 74 na Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ina asilimia 63.6. Takribani wananchi 528,939 kati ya wakazi 768,807 wanaoishi vijijini wanapata huduma hiyo.

Serikali imeeleza kuwa itaendelea kusimamia ukusanyaji wa madeni ya maji pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma ya maji safi, salama na endelevu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso