Serikali Yatahadharisha Vijana Kuhusu Athari za Kujiingiza Kwenye Vita vya Mataifa ya Nje
Serikali imetoa tahadhari kwa vijana wa Kitanzania kuhusu hatari na athari za kujiingiza katika migogoro ya kimataifa, ikiwemo vita baina ya nchi za Ukraine na Urusi, kutokana na madhara ya kiuchumi, kijamii, na kiusalama.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Jesca John Magufuli, Bungeni, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amebainisha kuwa kumekuwepo na mwenendo wa baadhi ya vijana barani Afrika kuhamasishwa kujiunga na majeshi ya nchi zenye vita kwa lengo la kutafuta kipato kutokana na changamoto za kiuchumi na uhaba wa ajira katika nchi zao za asili.
Serikali imesisitiza kuwa kujiingiza katika migogoro hiyo ni kinyume na sheria za nchi na za kimataifa, na kunaweza kugharimu maisha ya vijana kwa kusababisha vifo au ulemavu wa kudumu.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa kuzingatia Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001 Toleo la Mwaka 2024 na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, imeendelea kutoa elimu ya uraia na kujenga uelewa kwa vijana ili wasishawishike kujiingiza katika mapigano ya mataifa ya nje.
Hatua hizi zinalenga kulinda nguvu kazi ya taifa na kuhakikisha vijana hawajihusishi na vitendo vinavyokiuka miongozo ya kisheria na kidiplomasia ya Tanzania katika nyanja za kimataifa.
Ili kuwapatia vijana mbadala salama wa kujiingiza kwenye migogoro, Serikali kupitia Wizara imekuwa ikiratibu upatikanaji wa fursa za ajira nje ya nchi kupitia mikataba ya ushirikiano wa nchi mbili katika maeneo yenye mazingira salama ya kazi.
Katika mwaka huu wa fedha, jitihada hizo zimefanikisha upatikanaji wa nafasi 1,500 za ajira za udereva nchini Qatar na nafasi 300 za wauguzi nchini Saudi Arabia kwa ajili ya vijana wa Kitanzania.
Aidha, programu mbalimbali za ndani zinatekelezwa, ikiwemo utengaji wa Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo na programu maalum za kisekta zinazolenga kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za kiuchumi ndani ya nchi.

No comments:
Post a Comment