MBUNGE NGAYIWA AIPONGEZA SERIKALI KWA MIRADI YA BARABARA KAHAMA, AOMBA KUKAMILISHWA KWA BARABARA YA KAGONGWA–IGUSULE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 22 May 2026

MBUNGE NGAYIWA AIPONGEZA SERIKALI KWA MIRADI YA BARABARA KAHAMA, AOMBA KUKAMILISHWA KWA BARABARA YA KAGONGWA–IGUSULE


MBUNGE NGAYIWA AIPONGEZA SERIKALI KWA MIRADI YA BARABARA KAHAMA, AOMBA KUKAMILISHWA KWA BARABARA YA KAGONGWA–IGUSULE


Na Neema Nkumbi

Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha za kuboresha miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani, akisema hatua hiyo itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Akichangia bungeni mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Ngayiwa amesema serikali imetenga Shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya Kahama–Nyandekwa–Nyamilangano–Uyogu, hatua ambayo itarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa katika maeneo hayo.

Aidha, ameeleza kuwa barabara ya Kahama–Kakola–Buliankuru yenye urefu wa kilomita 73 nayo inaendelea kufanyiwa maboresho, huku barabara ya Kahama–Tulole–Mhulidede mpaka  Tabora yenye urefu wa takribani kilomita 152 ikitengewa fedha kwa ajili ya ukarabati. Pia kipande cha kilomita 20 kutoka Kahama hadi Tulole kimetengewa fedha za matengenezo.

Mbunge huyo ameishukuru Wizara ya Ujenzi kwa juhudi hizo, akisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya barabara una mchango mkubwa katika kukuza biashara, kilimo na huduma za kijamii kwa wananchi wa maeneo husika.

Hata hivyo, Ngayiwa ameiomba wizara hiyo kufanya juhudi za makusudi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Kagongwa–Igusule kwa kiwango cha lami ambapo amesema barabara hiyo yenye takribani kilomita 65 imefikia hatua nzuri ya maandalizi, huku kilichobaki kikiwa ni uwekaji wa tabaka la mwisho la lami.

Amesema kuwa kuchelewa kukamilisha mradi huo kunaweza kusababisha sehemu zilizojengwa kuharibika kutokana na mvua za msimu ujao, jambo ambalo litaongeza gharama za matengenezo na kuilazimu serikali kuanza upya baadhi ya kazi zilizokwisha kufanyika.

Katika mchango wake, Ngayiwa pia ameomba kasi iongezwe katika utekelezaji wa mradi wa barabara ya Kahama–Nyandekwa–Ng'wande–Ugala kuelekea Kaliua na Mpanda, ameeleza kuwa ni barabara muhimu inayounganisha mikoa mbalimbali na kusaidia usafirishaji wa mazao ya biashara na chakula ikiwemo tumbaku, mahindi, alizeti na mazao mengine.

Amesema wananchi wa maeneo hayo wanahitaji kuona hatua za utekelezaji zikianza kwa vitendo badala ya kuendelea kusikia taarifa za upembuzi yakinifu na usanifu pekee kila mwaka, akisisitiza kuwa ujenzi wa barabara hizo kwa kiwango cha lami utafungua fursa zaidi za kiuchumi na kurahisisha usafiri kwa wananchi katika kipindi chote cha mwaka.

#BungeTZ #BenjaminNgayiwa #KahamaMjini #WizaraYaUjenzi #BarabaraZaMaendeleo #SamiaSuluhuHassan #Kahama #Shinyanga

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso