Uchaguzi mkuu wa 2025 umeacha alama ya maumivu inayohitaji kutafakariwa kwa kina ili kuhakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa chombo cha kuimarisha demokrasia badala ya chanzo cha mifarakano.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman, ghasia zilizojitokeza hazikuwa tukio la ghafla, bali ni matokeo ya mrundikano wa changamoto za kisiasa na kijamii ambazo hazikupata majukwaa sahihi ya majadiliano. Katika mfumo wa vyama vingi, ushindani ni jambo la kawaida, lakini tatizo huanza pale maneno yanapotumika kama silaha ya kuchochea chuki badala ya kujenga hoja za kimaendeleo.
Ili kuepuka migogoro ya baadaye, taifa linapaswa kuimarisha utamaduni wa mazungumzo kati ya wadau wote wa siasa, viongozi wa dini, na asasi za kiraia. Ripoti inasisitiza kuwa matumizi ya lugha kali na kaulimbiu zinazohamasisha ukaidi dhidi ya mamlaka yalichangia kwa kiasi kikubwa kuwapa hamasa washiriki wa ghasia.
Funzo la msingi hapa ni kuwa viongozi wana wajibu wa kimaadili wa kuelekeza wafuasi wao katika njia za amani, na kwamba njia pekee ya kudumisha utulivu ni kuhakikisha kila upande unajihisi kusikilizwa katika meza ya majadiliano badala ya mitaani.
Kwa kuwa Ripoti ya Tume imebainisha kuwa ghasia za mwaka 2025 ziliacha majeraha makubwa moyoni mwa jamii, huku lugha kali za kisiasa zikitajwa kama kichocheo kikubwa; Kaulimbiu zenye mlengo wa mivutano zilizotumiwa na baadhi ya viongozi zikijenga uhasama badala ya ushindani wa kifikra,katika kuelekea mustakabali mwema, falsafa ya Maridhiano (Reconciliation) ni nguzo muhimu.
Ni lazima viongozi wa kisiasa, dini, na asasi za kiraia kukaa pamoja na kujenga utamaduni wa mazungumzo (Dialogue).
Tunahitaji majukwaa salama ambapo tofauti za kisiasa zinajadiliwa kwa staha bila kuhatarisha amani ya nchi.
Kama ripoti inavyosisitiza, "kutibu majeraha" ya kitaifa kunahitaji kila upande kukubali wajibu wake na kuweka mbele maslahi ya Tanzania. Hii itahakikisha kuwa chaguzi zijazo zinakuwa huru, za haki, na zinazozalisha viongozi bila kuacha taifa likiwa limepasuka vipande vipande.
No comments:
Post a Comment