
Askari wa kituo cha jeshi la zimamoto na uokoaji Kahama, wakifanya zoezi la maokozi kwa majeruhi wa ajali ya barabarani, katika kuimarisha uwezo wao wa kukabiliana na majanga ya moto na maokozi, kuongeza ufanisi, weledi na utayari wa kiutendaji. (Picha na zimamoto Kahama)
Na mwandishi wetu - Kahama
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga kupitia Kituo cha Wilaya ya Kahama, leo limeendelea kuimarisha uwezo wa askari wake katika kukabiliana na majanga ya moto na maokozi kwa lengo la kuongeza ufanisi, weledi na utayari wa kiutendaji.
Katika mazoezi hayo yaliyoongozwa na Mkuu wa Kituo hicho mkaguzi msaidizi Hafidhi Omari, askari walifanya mazoezi ya nadharia na vitendo ya kukabiliana na majanga ya moto na maokozi.
Omari ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Askari umuhimu wa kufanya mazoezi mara kwa mara, ili kuongeza uwezo, umakini na utayari wa kukabiliana na majanga ya moto na uokoaji kwa ustadi na ufanisi wa hali ya juu.
Katika zoezi la kwanza askari wameonyesha umahiri wa kukabiliana na majanga ya moto baada ya kupokea taarifa kupitia namba ya dharura ya jeshi hilo ambayo ni 114.
Zoezi la pili askari wameonyesha umahiri wa kufanya maokozi kwenye ajali baada ya kupokea taarifa kupitia kituo cha taarifa cha jeshi hilo kwenye namba 114.
Hata hivyo Omari anaeleza kuwa kituo cha zimamoto na uokoaji wilayani Kahama, lina vifaa vyote vya maokozi ikiwemo gari ya kubebea wagonjwa (Ambulance), endapo ikitokea ajali.
Amesema "Niwaombe wananchi kuendelea kuitumia vyema namba 114 kutoka taarifa zote za majanga na maokozi, gari ya wagonjwa tunayo pamoja na vifaa vingine vya maokozi, wasisite wapige simu watoe maelekezo sahihi tutafika kwa wakati."
Mkazi wa Kahama Agnes Kessy amesema "Nalipongeza sana jeshi la zimamoto kwa juhudi hizi, mwanzo wakati napita sikuwaza kama ni mazoezi ila niliposogea na kwa kuwa nina elimu kidogo nikagundua kinachoendelea. Hii itasaidia kuweka awareness kwenye jamii kuhusu majanga mbalimbali na maokozi."




No comments:
Post a Comment